Na Silivia Amandius.
Kagera.
Waandishi wa habari mkoani Kagera wamepewa elimu juu ya ugonjwa wa Marburg na kuhamasishwa kuzingatia usalama wao pamoja na kuandika habari za kitaalamu ili kuepusha taharuki kwa jamii.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Hajjat Fatma Mwasa, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika semina hiyo, amewataka waandishi wa habari kuhakikisha wanaripoti kwa weledi na kwa uhakika. Amesisitiza kuwa waandishi wa habari ni daraja muhimu katika kufikisha taarifa sahihi kwa wananchi ili kusaidia kukabiliana na ugonjwa huo kwa maslahi ya mkoa na taifa kwa ujumla.
“Hakikisheni habari zenu zinasaidia kuelimisha jamii na sio kusababisha taharuki. Pia, jihadharini na mazingira mnayofanyia kazi ili kujilinda na maambukizi,” alisema Mhe. Mwasa.
Aidha, mkuu huyo wa mkoa amewataka wananchi kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huo kwa kuepuka misongamano isiyo ya lazima, hasa kwenye mikusanyiko kama misiba na sherehe, hali inayoweza kuchochea kuenea kwa maambukizi.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Bi. Edna Moturi, ameahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania pamoja na wizara ya afya ili kuimarisha mapambano dhidi ya magonjwa ya mlipuko kama Marburg.
Naye Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya, Bw. Ntuli Kapologwe, amesema kuwa elimu kwa wananchi ni silaha muhimu katika kupambana na imani potofu zinazoweza kuhatarisha juhudi za kudhibiti ugonjwa huo.
Ikumbukwe kuwa ugonjwa wa Marburg ulitangazwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 20 Januari 2025 baada ya kuthibitishwa kwa kisa cha kwanza cha ugonjwa huo wilayani Biharamulo, mkoani Kagera.
Jamii inahimizwa kuendelea kuchukua tahadhari na kufuata miongozo ya wataalam wa afya ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Marburg.