Msimamizi wa mradi wa maji wa Miji 28 unaotekelezwa katika eneo la Chandamali Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma Mhandisi Vicent Bahemana ,akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo leo kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas kushoto,katikati Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya maji na usafi wa Mazingira Manispaa ya Songea Mhandisi Patrick Kibasa.
Msimamizi wa mradi wa maji wa Miji 28 unaotekelezwa katika eneo la Chandamali Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma Mhandisi Vicent Bahemana,akimuonyesha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas mchoro wa mradi huo unaotekelezwa katika eneo la Chandamali Manispaa ya Songea kwa gharama ya Sh.bilioni 145.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas,akikagua mradi wa maji eneo la Chandamali unaojengwa kwa gharama ya Sh.bilioni 145 unaotekelezwa na Serikali ili kuboresha Huduma ya maji katika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma.
Na Muhidin Amri,
Songea
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Ahmed Abbas,amemtaka Mkandarasi Kampuni ya China Civil Engineering Contruction Corporation(CCECC) kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji wa miji 28 kabla ya mwezi Oktoba mwaka 2025.
Abbas ametoa agizo leo,baada ya kukagua mradi huo unaotekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Maji ili kuboresha huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa Manispaa ya Songea na maeneo mengine ya jirani.
Alisema,lengo la Serikali kujenga miradi hiyo ili kuwezesha Wananchi kupata huduma ya maji badala ya kuwa mapambo,kwa kuwa baadhi ya maeneo Wananchi wanauhitaji mkubwa wa huduma ya maji.
“wito wangu kwa Mkandarasi endelee kufanya kazi ndogo ndogo kwa fedha zako,kazi zinazohitaji fedha za Serikali utasubiri na zitakapoletwa hakikisha unafanya kazi usiku na mchana ili mradi huo ukamilike na wananchi wapate maji”alisema.
Akiongeza kwa njia ya Simu Katibu Mkuu wa Wizara ya maji Mhandisi Mwajuma Waziri alisema,kusimama kwa ujenzi wa mradi huo kunatokana na madai ya fedha ya Mkandarasi,lakini baada ya wiki mbili fedha zitapatikana.
“kulikuwa na madai mengi ya fedha za miradi ya maji ikiwemo miradi ya miji 28,lakini Serikali imeanza kulipa madai ya Wakandarasi waliotangulia kuleta maombi yao na tutaendelea tulipa madeni mengine ya Wakandarasi wetu ”alisema.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji na usafi wa mazingira Manispaa ya Songea (Souwasa) Mhandisi Patrick Kibasa alisema,mradi ulianza kutekelezwa mwezi Januari 2024 na unatarajia kukamilika mwezi Septemba 2026.
Alisema,tayari Serikali kupitia wizara ya maji imeshamlipa mkanadarasi fedha za malipo ya awali kiasi cha Sh.bilioni 21.87 kati ya Sh.bilioni 145.77 ambazo zimepangwa kutumika kutekeleza mradi huo.
Alitaja kazi zilizopangwa katika mradi huo kujenga chanzo cha maji katika Mto Njuga chenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 17 kwa siku,ujenzi wa mtambo wa kuchuja na kutibu maji lita milioni 16 na kujenga matenki matatu yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 9.
Kibasa alitaja kazi nyingine zitakazotekelezwa ni kulaza bomba za kusambaza maji urefu wa kilometa 30.2,upanuzi wa mtandao wa bomba za usambazaji maji kilometa 34.7 kukarabati mtambo wa kuchuja na kutibu maji lita milioni 11.5 ambao kwa sasa ufanisi wake upo chini ya kiwango ili kukidhi mahitaji.
“mpaka sasa mkandarasi amekamilisha ujenzi wa matenki mawili kati ya matatu yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 2 ambayo ni tenkiyamejengwa eneo la Chandamali na Milaya na tenki la Mahilo la lita milioni 5 lipo katika hatua za uchimbaji wa msingi”alisema.
Alisema,mpaka kufikia tarehe 30 Novemba mwaka jana utekelezaji wa mradi umefikia asilimia zaidi ya 5 utawezesha kuboresha huduma za maji safi na usafi wa mazingira kwa Wakazi wa Manispaa ya Songea.