Mhandisi wa TARURA Wilayani Tunduru Msola Julius kulia,akiwaangalia mafundi wanaojenga Daraja katika Barabara ya Mchoteka-Likweso-Wenje ambapo Serikali imetoa kiasi cha Sh.milioni 480 kwa ajili ya kufungua Barabara hiyo.
Na Mwandishi Maalum,
Tunduru
WAKAZI zaidi ya 6,600 wa vijiji vya Mchoteka,Likweso na Wenje wilayani Tunduru,wameondoka na changamoto ya kukosa mawasliano ya baada ya Serikali kutoa shilingi milioni 480 zilizotumika kufungua Barabara mpya inayoungunisha vijiji hivyo.
Mhandisi wa TARURA wilaya ya Tunduru Msola Julius alisema,awali Barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 24 haikuwepo hivyo wananchi walishindwa kuwasiliana kwa njiaa ya barabara na kufanya shughuli za kiuchumi,usafiri na usafirishaji wa mazao hasa Korosho,Karanga na Mpunga yanayolimwa kwa wingi katika maeneo hayo.
Alisema,Barabara hiyo imeanza kupitika na kazi zinazoendelea ukutekelezwa katika mradi huo ni ujenzi wa mitaro ya kupitisha maji pande zote mbili yenye urefu wa kilometa 1.6,makalavati na daraja.
Alisema,mradi huo ulianza kutekelezwa tarehe 29 Mei 2024 na utakamilika tarehe 24 mwezi huu na ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizofanikisha kuifungua Barabara hiyo.
Alisema,Barabara hiyo ni muhimu siyo kiuchumi tu bali hata kiulinzi kwani vijiji hivyo vinapataka na nchi jirani ya Msumbiji na itatumika kuharakisha maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Mkandarasi wa mradi huo kutoka Kampuni ya ARICOM ENTERTRADE Abdulrahman Soud alisema, mradi ulikuwa na sehemu mbili ambapo katika sehemu ya kwanza ni kuifungua Barabara na sehemu ya pili kujenga miundombinu.
Alisema,kazi zilizopangwa kutekelezwa katika sehemu ya kwanza ambazo zilikuwa kumwaga kifusi na kujenga makalavati 12 zimekamilika sasa wanamaliza sehemu ya pili kujenga daraja ambalo litakamilika baada ya wiki mbili.
Kwa mujibu wa Soud, Barabara hiyo ina umuhimu mkubwa, kwani kwa muda mrefu wananchi wa vijiji hivyo vitatu hawakuwa na mawasiliano ya uhakika,lakini kufunguliwa kwa barabara hiyo ni fursa kubwa kwa sababu wataitumia kuwasiliana,kusafiri na kusafirisha mazao wanayolima.
Mkazi wa kijiji cha Mchoteka Omari Malenga alisema,kabla ya ujenzi wa barabara hiyo changamoto kubwa ilikuwa maji ya mvua yanayotoka barabarani na kuelekea kwenye makazi yao na kushindwa kusafirisha mazao kutoka shambani kupeleka sokoni.