Watumishi na wadau mbalimbali wa Mahakama Wilayani Tunduru Mkoa wa Ruvuma,wakielekea kwenye viwanja vya Baraza la Idd wilayani humo kabla ya uzinduzi wa wiki ya Kisheria iliyofanyika jana nchini kote.
Na Mwandishi Wetu,
Tunduru
WATUMISHI na wadau wa Mahakama katika Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma,wamefungua wiki ya Sheria kwa kufanya matembezi ya kilometa moja yaliyoongozwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi wa Wilaya Shughuli Mwampashe na kupokelewa na Katibu Tawala wa wilaya hiyo Milongo Sanga.
Akizungumza na Watumishi,Wadau na Wananchi waliodhuria uzinduzi wa wiki ya Sheria kwa mwaka 2025 katika viwanja vya Baraza la Idd mjini Tunduru,Katibu Tawala wa wilaya hiyo Milongo Sana,amewataka Wananchi kutumia wiki ya sheria kufika kwenye maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili ya kutoa huduma za kisheria ili kupata utatuzi wa changamoto walizonazo.
Sanga alisema,Serikali kupitia Mhimili wa Mahakama imetenga vituo saba ambavyo wataalam wa sheria wakiwemo Mahakimu watakuwepo kwenye vituo ili kusaidia jamii kupata msaada wa kisheria kuhusiana na matatizo mbalimbali kwenye maeneo wanayoishi.
Sanga amevitaja vituo vitakavyotumika kutoa msaada wa kisheria kwa Wananchi wa Tunduru na Watanzania kwa ujumla ni Shule ya Sekondari Frank Weston,Mataka,Mgomba,Shule ya Msingi Mchangani,Mhule ya Msingi Umoja na Chuo cha ufundi Mbesa.
Aidha alisema,huduma ya kisheria itafikishwa kwa viongozi wa Dini kupitia nyumba za ibada ili nao waweze kupata uelewa kwa sababu ni viongozi katika jamii na wanakutana na changamoto nyingi ambazo zinafikishwa na waumini wao.
Amemshukuru Rais Samia Suluhu Suluhu Hassan,kwa kuboresha huduma za Mahakama hapa Nchini ikiwemo kuanzishwa kwa Mahakama mtandao ambayo imesaidia wananchi kupata elimu na taarifa mbalimbali.
Hata hivyo,amewaomba Watumishi wa Mahakama,(Mahakimu na watendaji wengine) kuhakikisha wanatenda na kutoa haki sawa kwa Wananchi wanaofika kwenye maeneo yao ya kazi bila kujali cheo wala nafasi ya mtu katika jamii.
“msingi wa maendeleo na ustawi wa jamii sehemu yoyote ni amani na hakuna amani pasipo na haki,hivyo nawaomba sana watumishi wa Mhimili huu wa Nchi muendelee kutenda haki kwa wananchi”alisisitiza Sanga.
Kwa upande wake Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi wa Wilaya ya Tunduru Shughuli Mwampashe alisema,lengo la kuwa na wiki ya sheria ni kuwapa Wananchi uelewa ili wafahamu mambo mbalimbali yanayofanywa na Mahakama na wadau wake.
Alisema,katika wilaya hiyo mashauri mengi yanayofikishwa Mahakamani ni Ubakaji na Uhujumu Uchumi ambapo amewasisitiza Wananchi kuwa na tabia ya kutembelea maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya kuwapa elimu na kutoa msaada wa Sheria.
Naye Mdau wa Sheria kutoka kituo cha Msaada wa Sheria cha TUPASE Wilayani humo John Nginga alisema,changamoto iliyopo kwa jamii ni kukosa uelewa kuhusiana na upatakanaji wa haki zao za msingi na hawafahamu watazipata wapi.
“Unaweza kujua haki zako za msingi kisheria lakini namna unavyozidai unaweza kujikuta unavunja sheria na baadaye unaingia kwenye mikono ya sheria na kupata matatizo makubwa”alisema Nginga.