Na. Faraja Mbise, DODOMA
Walimu wakuu kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma wamepatiwa mafunzo juu ya ununuzi kwa njia ya mtandao serikalini yatakayoboresha utendaji kazi na kuwawezesha kupata mafundi na watoa huduma kupitia mfumo wa ununuzi ‘National e-Procurement System of Tanzania’ yaani ‘NeST’.
Mafunzo hayo yameanza leo tarehe 21 Januari, 2025 na Kitengo cha Ununuzi na Ugavi cha Halmashauri ya Jiji la Dodoma, kwa walimu wakuu wa shule za msingi katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Umonga.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi, Vincent Odero alisema kuwa mfumo wa manunuzi serikalini kwa njia ya kielektroniki ni mfumo mzuri na umerahisisha mchakato mzima wa manunuzi na umeleta ufanisi mkubwa katika ununuzi wa umma katika maeneo mbalimbali. “Mfumo huu ni mzuri, umerahisisha mchakato wa ununuzi ambapo taratibu zote za ununuzi hufanyika ndani ya mfumo. Mfumo huu umeleta ufanisi katika ununuzi wa umma kupitia maeneo mbalimbali” alisema Odero.
Kuhusu umuhimu wa mfumo wa ununuzi serikalini, alieleza namna ambavyo mfumo umerahisisha utendaji kazi tofauti na mfumo uliokuwa unatumika awali. “Mfumo wa ununuzi umeongeza uwazi na usawa katika mchakato wa ununuzi, kila mzabuni ana haki sawa ya kuwasilisha zabuni na umepunguza muda wa mchakato wa zabuni. Hivyo, kusaidia ununuzi kufanyika kwa muda mfupi, umepunguza mianya ya rushwa, umeboresha utunzaji wa taarifa za michakato ya ununuzi, umeongeza uwajibikaji kwa watumishi wa umma kwasababu mfumo unaonesha kila hatua ya ununuzi na kupunguza gharama za michakato ya zabuni kwa taasisi na wazabuni” alisisitiza Odero.
Sanjari na hayo alielezea kuhusu agizo la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Waraka wa Hazina Namba 2 wa Mwaka 2023/2024, alisema kuwa, unaelekeza watumishi wote wa umma wanahusika na mchakato wa ununuzi ndani ya taasisi za serikali kupatiwa mafunzo yatakayowawezesha watumishi kutumia mfumo wa NeST kwa ufasaha. “Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo tarehe 27 Julai, 2023 ilitoa Waraka wa Hazina Namba. 2 wa Mwaka 2023/24 kuhusu matumizi ya mfumo wa usimamizi wa ununuzi wa umma kwa njia ya kielekroniki ‘NeST’, ambao ulielekeza kwamba, watumishi wote wa umma wanahusika na mchakato wa ununuzi ndani ya taasisi za serikali wapewe mafunzo yatakayowawezesha kutumia mfumo kwa ufasaha. Halmashauri ilitekeleza jukumu hilo kwa kuwawezesha maafisa ununuzi na ugavi kupata mafunzo hayo” alisema Odero.
Aidha, aliwataka walimu wakuu kutokiuka sheria, kanuni na miongozo inayotolewa na Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA). “Kaguzi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) na za Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) zinazofanyika kila mwaka, zimebaini kuwepo kwa mapungufu katika taratibu za ununuzi unaofanyika ikiwemo ukiukwaji wa sheria, kanuni na miongozo inayotolewa. Mapungufu haya yamekuwa ni sababu kubwa ya upotevu wa fedha za serikali na miradi mingi kushindwa kukamilika na iliyokamilika kutokuwa na ubora unaotakiwa. Hivyo, niwaombe kufuata kanuni na taratibu zinazotolewa na Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Unuuzi wa Umma (PPRA) alisisitiza Odero.
Mkuu huyo wa kitengo alisema kuwa katika mafunzo hayo washiriki watafundishwa kuandaa mpango wa ununuzi wa mwaka, kuanzisha manunuzi kwenye mfumo, kuandaa nyaraka za zabuni kwenye mfumo. Maeneo mengine ya mafunzo aliyataja kuwa ni kufanya ufunguzi wa zabuni kwenye mfumo, kufanya tathmini kwenye mfumo, kutunuku zabuni kwenye mfumo na kuandaa mkataba kwenye mfumo, aliongeza.
Vilevile, aliongeza kwa kusema kuwa, watumishi hao wameaminiwa na kukabidhiwa na serikali jukumu la kufanya na kusimamia ununuzi wa umma katika vituo vyao vya kutolea huduma. Pia alisema kwa atakaekiuka sheria na kanuni hatua kali za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni faini ya shilingi 10,000,000 kwenda jela miaka mitatu au vyote kwa pamoja.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeandaa mafunzo kwa mara nyingine kwa watumishi wote kutokana na maelekezo ya serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa halmashauri zote nchini kutumia ‘NeST App’ kwa manunuzi yote yanayofanyika ofisi kuu na katika vituo vya kutolea huduma.