Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Daniel Chongolo akitoa za wadi kwa mmoja wa washindi waliofanya vizuri kwenye matokeo ya darasa la saba mwaka 2019,wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Kinondoni. Mhe. Harlod Muruma.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Daniel Chongolo, akizungumza na walimu, watendaji wakati wa hafla ya kuwapongeza walimu kwa matokeo mazuri ya kumaliza elimu ya msingi mwaka 2019. kulia ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni Mhe. Harlod Muruma na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Dk. Patricia Henjewele.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Daniel Chongolo akizindua zoezi la utoaji tuzo kwa ngazi ya Kata utakaofanyika leo . wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni Mhe. Harlod Muruma, wanaoshuhudia tukio hilo kushoto ni Kaimu Afisa elimu wa Halmashauri hiyo, Bi Chitegets Dominick, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Dk. Patricia Henjewele.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Daniel Chongolo, akionyesha zawadi aliyotunukiwa na Idara ya Elimu kuonyesha mchango wake katika sekta hiyo, kulia ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni Mhe. Harlod Muruma na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Dk. Patricia Henjewele.
********************************
Mkuu Wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Daniel Chongolo amewaagiza wakuu wa shule zote za Sekondari katika Halmashauri hiyo kuacha mara moja tabia ya kuwazuia wanafunzi wanaojiunga na kidato cha chanza kuanza maso kutokana na kutokamilisha mahitaji yao ya shule.
Mhe. Chongolo ametoa agizo hilo jana wakati wa hafla ya kuwapongeza walimu kwa ufaulu mzuri wa mitihani ya kumaliza elimu ya msingi mwaka 2019 iliyofanyika katika viwanja vya Polisi Officers Mess.
Mhe. Chongolo amefafanua kuwa zipo baadhi ya shule ambazo zinawazuia wanafunzi kujiunga na masomo kutokana na kutokamilisha mahitaji ya shule na kusema kuwa bado hajasikia jambo hilo likifanyika katika Halmashauri ya Kinondoni na hivyo kutumia nafasi hiyo kuwaonya wasithubutu kufanya hivyo.
Aliongeza kuwa Serikali ya awamu ya tano imetoa elimu bure bila malipo na kwamba suala la kuchelewa kukamilisha mahitaji hayo isiwe sababu ya kuwazuia watoto hao wa wanyonge kushindwa kuanza masomo yao.
“ Kuna baadhi ya maeneo nimesikia kuna wakuu wa shule wanawarudisha nyumbani watoto kwa sababu hawajakamilisha mahitaji yao, kama mtoto hana viatu, sijui nini waache wasome wakati wazazi wao wanawatafutia mahitaji hayo, naomba nisikie mwanafunzi amerudishwa nyumbani kwenye wilaya yangu” amesisitiza Mhe. Chongolo.
Mhe. Chongolo aliongeza kuwa mafanikio ya kufanya vizuri kwa wanafunzi wa darasa la saba mwaka 2019 kwenye Halmashauri hiyo ni uthibitisho tosha unao onysesha namna walimu, wazazi na wanafunzi katika wanashirikiana kikamilifu katika nyanja ya elimu na hivyo kutoa wito kwa wazazi kuendeleza ushirikiano huo katika usimamizi wa wanafunzi hususani kwenye masuala ya taaluma.
Alisema ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ilianzisha mkakati wa ujenzi wa madarasa 100 ambapo kwa shule ya Sekondari ni madarasa 40 huku shule ya msingi madarasa 60 lengo likiwa ni kuongeza tija katika taaluma na kupunguza changamoto ya miundombinu inayoikabili shule hizo na kwamba jumla ya vyumba 24 vya madarasa kwa shule ya msingi zipo katika hatua ya ukamilishaji.
Mhe. Chongolo alitumia nafasi hiyo kumpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo , Ndugu Aron Kagurumjuli kwa usimamizi mzuri wa elimu na kwamba anatambua jitihada zake za kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanapata elimu bure na kwamba anatimiza kimamilifu majukumu na maagizo yanayotolewa na Rais Dk. John Magufuli.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Halmashauri hiyo, Benjamini Sita alisema kuwa hafla hiyo ni mahususi kwa ajili ya kuwapongeza walimu kwa kuwa Halmashauri hiyo imekuwa kwenye nafasi ya tatu kitaifa katika matokeo ya darasa la saba na kwamba inajipanga kuhakikisha kuwa inashika nafasi ya kwanza kitaifa katika matokeo ya mtihani ijayo.
Aidha Kaimu Afisa elimu wa Halmashauri hiyo, Bi Chitegets Dominick alieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na uongozi mahiri wa Mstahiki Meya Benjanimi Sita, Mkurugenzi Aron Kagurumjuli kwa kushirikiana na watendaji wa Idara ya Elimu na Idara nyingine na hivyo kumhakikishia Mhe. Chongolo kuwa watahakikisha wanafanya vizuri zaidi katika mitihani ijayo.
Aliongeza kuwa Halmashauri hiyo imefanya vizuri katika mtihani wa darasa la saba mwaka 2019 kwa kuwapa ufaulu wa asilimia 97.17 ambapo imekuwa ya tatu kati ya Halmashauri 186 kitaifa kwa jumla ya wanafunzi waliosajiliwa kufanya mtihani huo walikuwa 12,619, wavulana 6,115 na wasichana 6,450, huku walioganya wakiwa 12,523 ,wavulana 6,058 na wasichana 6,465.