Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Augustine Mahiga(Mb) Akiongea na Wanahabari jijini Dar es Salaam leo.
******************************
Tanzania imekuwa miongoni mwa wanachama walionufaika na ARINSA kwa kujiunga na umoja huo ikiwa ni pamoja na watendaji wa haki za jinai wakiwemo waendesha mashtaka kupata mafunzo kwa vitendo kwenye taasisi za serikali za nchi nyingine kwa ajili ya kujifunza na kubadilishana uzoefu.
Ameyasema hay oleo Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Augustine Mahiga (Mb) katika utoaji wa taarifa juu ya maadhimisho ya Miaka 10 ya Umoja wa Taasisi zinazokabiliana na uhalifu unaovuka mipaka kwa kutumia dhana ya utaifishaji na urejeshaji mali zitumikazo au kutokana na uhalifu kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Waziri huyo amesema kuwa Umoja huo ambao sasa una nchi wanachama 16, ulianzishwa mwezi Machi, 2009 nchini Afrika Kusini baada ya mkutano uliojumuisha wawakilishi wa taasisi za mashtaka na upelelezi wa makosa ya jinai kutoka nchi tisa za Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania, Botswana, Lesotho, Mauritius, Namibia , Afrika Kusini, Swaziland (sasa Eswatini), Zambia na Zimbabwe walikutana na kujadili namna bora ya kukabiliana na uhalifu mkubwa unaovuka mipaka kwa kutumia dhana ya utaifishaji na urejeshaji wa mali zinazohusiana na uhalifu.
“Tanzania kama nchi Mwenyeji imeanza kupokea wageni kutoka katika nchi hizo hivyo ni matarajio yetu kuwa tutaitumia fursa ya ujio wa ugeni huo kuitangaza nchi yetu na vivutio vya utalii vyake ambavyo tumebarikiwa kuwa navyo na hivyo kuwafanya wageni hao kurudi tena nchini kwa ajili ya kuitembelea nchi yetu”. Amesema Dkt. Mahiga.
Aidha Dkt. Mahiga amesema kuwa hatua hiyo iliyokana na ukweli kwamba, kwasasa duniani kote imekubalika kuwa utaratibu uliozoeleka wa kutoa adhabu za vifungo kwa wahalifu sio njia madhubuti ya kuzuia uhalifu na badala yake imethibitika kuwa utaifishaji wa mali zinazohusiana na uhalifu ndiyo madhubuti Zaidi ya kuzuia uhalifu.
“Lengo la Umoja huu ni kuwa na ushirikiano wa karibu wa kitaasisi baina ya nchi wanachama kwa lengo la kuhakikisha kuwa wahalifu hawafaidiki na mali zinazohusiana na uhalifu na hawana mahali pa kujificha katika nchi wanachama”. Amesema Dkt. Mahiga.
Maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika Juni 12 mwaka huu katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere (JNICC) na inatarajiwa kuwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu ambaye atakuwa ni mgeni rasmi.