Mtaalam wa Taasisi ya Tiba na Mifupa-MOI akishiriki zoezi la kutoa damu kwa mmoja wananchi waliojitokeza leo.
Afisa Habari wa Taasisi ya Chakula na Lishe Jackson Monela (wa kwanza kulia) akishiriki katika zoezi la kuchangia damu leo katika zoezi linaloendelea MOI ambapo wadau mbalimbali wamejitokeza.
…………..
KAMPENI ya Tumeboresha Sekta ya afya imeongeza hamasa kubwa kwa Wananchi na wadau kujitokeza kwa wingi kuchangia damu ambapo sasa Taasisi ya Tiba ya Mifupa-MOI inaweza kukusanya chupa za damu zaidi ya 150 kwa siku
Kampeni hiyo ambayo kwa mwaka huu ni awamu ya pili, imekuja kwa wakati muafaka ambapo wadau wa Asasi ya Family Federation for World Peace (FFWP) wamekuwa wakileta wachangia damu 1000 kwa siku.
“Tupo katika kampeni ya Tumeboresha Sekta ya Afya. Ambapo pia tuliweza kutumia nafasi hii kuhamasisha wananchi wajitokeze kwa wingi kuchangia damu hapa MOI na muitikio umekuwa mkubwa na tunapata damu kuanzia chupa zaidi ya 100 kwa siku na hii ni faraja kubwa sana kwetu” alisema Afisa Habari na Mahusiano MOI, Patrick Mvungi.
Mvungi aliongeza kuwa, Asasi hiyo ya FFWP imeshaleta wananchi 1500 huku siku ya kwanza ikileta wananchi 1000 na siku ya pili Wananchi 500 na wanatatajia kumalizia 500 wengine.
Aidha. Mvungi amebainisha kuwa, kwa upatikanaji huo wa damu kwa sasa hakuna mgonjwa anayekosa kufanyiwa upasuaji kwani kuna damu ya kutosha.
“Mahitaji ya damu MOI kwa siku ni chupa 15 hadi 30. Kabla ya zoezi ili la kuchangia damu, kwa siku tulikuwa tunapata chupa chini ya 15 na zilikuwa zinatoka Mpango wa Taifa wa Damu Salama na Wananchi wachache waliokuwa wanakuja kujitolea.
Kampeni ya Tumeboresha Sekta ya Afya inaendeshwa na Maafisa Habari waandamizi kutoka Wizara ya Afya na Taasisi zake ambapo kampeni hiyo itakuwa endelevu na Watanzania wanahamasishwa kujitokeza kuendelea kuchangia damu kwa wenye mahitaji.