Mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa kupitia chama cha mapinduzi (CCM) Rose Tweve akisisitiza jambo wakati wa barza la UWT wilaya ya Iringa Vijijini
Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Iringa Vijijini Lenah Hongoli akizungumzia namna ya kuendeleza umoja na kukijenga chama na kuongeza wanachama kwenye umoja huo
NA FREDY MGUNDA, IRINGA
WANACHAMA wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Iringa Vijijini wametakiwa kuwa na ushirikiano, mshikamano na upendo kwa lengo la kudumisha amani iliyopo nchini katika kuendeleza mazuri yaliyoasisiwa na wazee wa taifa wakiongozwa na baba wa Taifa Mwalimu Julias Kambarage Nyerere.
Akizungumza kwenye baraza la UWT wilaya ya Iringa vijijini, mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa Rose Tweve alisema kuwa wanatakiwa kuendeleza utamaduni wa kushirikiana kuhakikisha wanajenga nchi na chama hicho kwa lengo la kuendelea kushika dola na kuacha siasa za kuchukiana.
Alisema kuwa endapo wanachama watadumisha upendo,mshikamano na umoja nchi itaendelea kuwa na amani ambayo imedumu tangu kupatikana kwa uhuru na kuongeza kuwa wanachama wanatakiwa kukijenga chama kwa umoja wao.
Aidha Tweve alisema kuwa wameibuka baadhi ya wanachama mkoa wa Iringa wanaoeneza maneno ya chuki kwenye vikundi vya kukuza uchumi vya kila kata ambavyo vilianzishwa kwa lengo la kuwakomboa wanawake wa UWT mkoa wa Iringa hali ambayo haependezi na kuwataka kukuza chama na uchumi wa vikundi kuliko kuendeleza vitu visivyo na maana.
“Kuna watu wanataka ubunge hivyo wameanza kunichafua mimi kupitia vikundi ambavyo nilivianzisha kwa lengo zuri la kumkomba wanamke kiuchumi na sikuwa na lengo jingine hivyo hata wao wananafasi ya kufanya hivyo lakini sio kunichafua kisiasa” alisema
Aliongeza kuwa mtu yoyote mwenye nia ya kuwaletea maendeleo wanawake wanaruhusiwa lakini sio kwa kuja na mbinu ya kuchafua wengine kwa lengo la kuleta chuki na endapo unahitaji kufanya jambo basi jitahidi kuleta jambo lenye manufaa kwa wanachama na liwe jipya kwao.
Tweve alisema kuwa wakati ni sasa wa kufanya maendeleo kwani maisha hayamsubiri mtu hivyo ni jukumu la kil mwanamke kujiunga katika vikundi vya ujasiliamali kuweza kujikomboa na hali ngumu ya kiuchumi.
Alisema kuwa maendeleo ya nchi yanategemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa wanawake kwani nguzo katika kuzalisha hivyo mwanamke asibweteke katika kutafuta shughuli ya kufanya ni muhimu kujiunga katika vikundi ambavyo vinawezesha wengi kujikomboa kutoka katika umaskini.
Vilevile alisema kwamba umoja na mshikamano ndio nguzo ya maendeleo na kujikomboa kiuchumi kwa kwa wanawake nchini hivyo ni muhimu sana kwa mwanamke kushirikiana na kufanya shughuli kwa pamoja kuliko kujitenga na kuanzisha maneno yasiyo na tija.
Naye mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Iringa Vijijini Lenah Hongoli alimpongeza mbunge huyo kwa jitihada ambazo amekuwa akizifanya kuhakikisha anawakomboa wanawake kiuchumi kwa kuwapa mtaji wa kuanza kukopeshana kwa ajili kufanya shughuli za kibiashara.
Alisema kuwa vikundi vindi vilivyoanzishwa na mbunge Rose Tweve vimefanikiwa kukuza mitaji na kufanya shughuli za maendeleo kwa mtu moja moja hiyo ni hatua kubwa sana kimaendeleo kwa wanawake wa wilaya ya Iringa Vijijini.
Hongoli aliongeza kwa kusema kuwa wanachama wa chama cha mapinduzi wanapaswa kuwa na mshikamano ili kuhakikisha wanaongeza wanachama na kuendelea kuimalisha na kukidumisha chama hicho.