WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda.akizungumza waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Januari 10,2025 jijini Dodoma kuhusu uzinduzi Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023 na Mitaala ilivyoboreshwa utakaozinduliwa Januari 31, Mwaka huu kwenye ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete.Kushoto ni Naibu Waziri, Omar Kipanga,Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Carolyne Nombo.
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda.akizungumza waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Januari 10,2025 jijini Dodoma kuhusu uzinduzi Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023 na Mitaala ilivyoboreshwa utakaozinduliwa Januari 31, Mwaka huu kwenye ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete.
Na.Alex Sonna-DODOMA
RAIS Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023 na Mitaala ilivyoboreshwa Januari 31, Mwaka huu ambayo inalenga kumuandaa mwanafunzi kuwa na ujuzi na kuendana na dunia ya sasa ikiwamo matumizi ya Akili Mnemba.
Hayo yamesemwa leo Januari 10,2025 jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi huo ambao utafanyika jijini Dodoma kwenye ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete.
Amesema mageuzi hayo yanagusa vizazi na vizazi, na ukamilifu wa utekelezaji wake kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita utachukua muda na kwasasa umeanza kufanyika kwa awamu na kila mwaka mabadiliko yataonekana.
Aidha Waziri Mkenda amebainisha kuwa kwasasa wameanza hatua kwa hatua kwenye elimu ya awali, darasa la kwanza, la tatu, kidato cha kwanza na kusisitiza kuwa hatua hiyo ni kubwa na itabadilisha mwelekeo wa nchi katika suala la elimu.
Ameeleza kuwa kuna hoja mbalimbali ambazo zinazungumzwa na wadau na wananchi ambazo majibu yake yapo kwenye sera na mitaala mipya.
“Mfano kuna mjadala mkubwa unaoendelea kwa sasa ni kuhusu somo la Kiingereza ambalo kwenye sera suala la lugha lipo na kwenye mitaala ni ufundishaji wa lugha.”
“Tunasikia watu wanazungumza suala la Artificial Intelligence ni suala kubwa sana ukienda kwenye sera utaona masuala ya Tehama na mambo yote ya Tehama yaliyozungumzwa na ukija kwenye mitaala utaona utekelezaji wake unavyofanyika,”amesema Prof.Mkenda
Pia, amesema suala la sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati linazungumzwa sana na kwenye sera inabainisha namna inavyozingatiwa na mitaala inaeleza namna inavyotekelezwa.
Hata hivyo Waziri Mkenda amesema kuna masuala ya kumuandaa mwanafunzi, sio tu kwenye ubora wa elimu lakini kuwa na ujuzi unaomuandaa kwenye dunia ya sasa na mabadiliko makubwa yanayotokea duniani.
Amesema katika uzinduzi huo wadau na viongozi mbalimbali wamealikwa kwenye uzinduzi huo unaotarajiwa kuhudhuriwa na watu takribani 3,000 na kutakuwa na maonesho ya taasisi mbalimbali za elimu.
Amefafanua hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia aliyoyatoa alipohutubia Bunge ambapo aliahidi watanzania kwamba serikali anayoiongoza itahakikisha inafanya mageuzi makubwa ya sera ya elimu na mitaala.
Prof.Mkenda amesema kutokana na ahadi hiyo alitoa maelekezo mahsusi kwa Wizara ya Elimu kwa ajili ya kusukuma jambo hilo na mapitio ya sera na mitaala yamechukua takribani miaka mitatu.
“Kazi hii imefanyika kwa kushirikisha wadau mbalimbali ikiwamo wataalamu wa elimu, walimu, wanafunzi, wananchi na maoni yalipokelewa nyakati zote ili kuleta ufanisi kwenye mapitio haya na pia mchakato huo ulihusisha kujifunza kwenye nchi mbalimbali na walitembelea kwenda kuangalia wanachofanya kwenye elimu ili kupata mbinu za kuboresha elimu ya Tanzania,”amesema
Amesema ili kuleta ufanisi wa utekelezaji wa sera hiyo, serikali imeanza kuwapiga msasa walimu nchi nzima na inatajiri hivi karibuni walimu 4,000 somo la biashara.
Naye, Naibu Waziri, Omar Kipanga amesema jambo hilo ni kubwa na ni kiu ya watanzania kuona mageuzi hayo katika mfumo wa elimu nchini.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Carolyne Nombo,amevishukuru vyombo vya habari namna vinavyotoa taarifa kwa umma kuhusu mageuzi yanayofanywa na wizara hiyo na inavyotekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).