WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi amemaliza mgogoro baina ya Wamiliki wa Shamba la Sisal Estate na Wananchi 400 wa Kata ya Kwashemshi Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga uliodumu kwa zaidi ya miaka 30.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa eneo hilo, Mhe. Ndejembi amesema baada ya kufanya vikao na mwekezani huyo, makubaliano yalifikiwa ya kuwapatia wananchi hao ekari 100 kwa ajili ya Makazi na matumizi mengine ambayo yatapangwa na Halmashauri
“ Serikali hii ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan inajali ustawi wa Wananchi wake na Wawekezaji. Tumefanya vikao na wenzetu wa Sisal Estate na tumekubaliana kwa pamoja zitolewe ekari 100 kwa wananchi.
Hivyo ekari 70 zitatolewa kwa makazi ya wananchi na ekari 30 zitaenda kwa Halmashauri ili ziweze kupangiwa matumizi bora ya Ardhi. Wito wangu kwenu asijitokeze mwananchi mwingine kuja kuvamia, kila mmoja awe mlinzi wa mwingine ili tuepushe migogoro mingine,” Amesema Mhe Ndejembi.
Aidha Mhe. Ndejembi ametoa rai kwa wananchi nchini kuacha kuvamia maeneo ambayo tayari yana hati ili kuepusha migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini.