Baadhi ya wakulima wa mahindi katika kijiji cha Kigonsera wilaya y Mbinga,wakisubiri kupima mahindi kwenye kituo cha ununuzi cha Kigonsera.
Meneja wa wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula(NFRA)Kanda ya Songea mkoani Ruvuma Zenobius Kahere,akizungumza na baadhi ya wakulima wa mahindi katika kijiji cha Kigonsera wilayani Mbinga wakati wa msimu wa ununuzi wa mahindi uliomalizika mwezi Novemba mwaka huu,kushoto kwake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Mbinga Andrew Mbunda.
Wakulima wa mahindi kutoka vijiji mbalimbali wilaya ya Namtumbo wakisafisha mahindi yao kabla ya kuuza kwa wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula(NFRA)kituo cha Rwinga wilayani humo,kushoto ni msimamizi wa kituo hicho kutoka NFRA Thabitha Mpangala.
Na Mwandishi Wetu,Ruvuma
WAKALA wa Taifa wa hifadhi ya chakula(NFRA)Kanda ya Songea mkoani Ruvuma,imenunua tani zaidi ya 72,000 za mahindi kutoka kwa wakulima katika msimu wa kilimo 2024/2025.
Meneja wa Wakala wa Taifa wa hifadhi ya Chakula kanda ya Songea Zenobius Kahere amesema,mahindi hayo yamenunuliwa kupitia vituo 21 vilivyowekwa katika Halmashauri saba za mkoa huo isipokuwa wilaya ya Tunduru ambayo sehemu kubwa wananchi wake wanajishughulisha na kilimo cha zao la korosho.
Kahere alisema, kwa kuwa mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa iliyopewa hadhi ya kuwa ghala la Taifa kutokana na uwezo wake katika uzalishaji wa zao hilo na mazao mengine ya chakula na biashara,wakati mwingine NFRA inahudumia mikoa mingine yenye upungufu wa chakula hapa nchini.
“Tulifungua vituo vya ununuzi katika Halmashauri zetu saba kati ya nane na tuliweza kukusanya mahindi zaidi ya tani hizo elfu sabini na mbili,ilipofika mwezi Novemba vituo hivyo vilifungwa na kazi inayoendelea kwa sasa ni ukusanyaji na ubebaji wa mahindi hayo kutoka kwenye vituo na kupeleka kwenye maghala mbalimbali kwa ajili ya kuhifadhi”alisema Kahere.
Alisema,katika msimu wa mwaka huu wakulima wa mahindi walifurahia bei nzuri ya Sh. 700 iliyotolewa na Serikali ikilinganisha na bei ya watu binafsi ambaao walinunua kati ya Sh.300 hadi 450 kwa kilo moja.
Hata hivyo alisema, changamoto kubwa iliyojitokeza ni ubora wa mahindi yaliyopelekwa sokoni na wakulima kutoka katika maeneo mbalimbali kwani hayakuwa na ubora hivyo kukosa vigezo vilivyowekwa na NFRA.
Alisema,hali hiyo iliwalazimu wakulima kutumia muda mrefu kukaa kwenye vituo vya ununuzi kwa ajili ya kusafisha na kuchagua ili kupata mahindi yenye ubora kabla ya kupokelewa na kupimwa.
Alisema kutokana na changamoto hiyo, katika msimu wa kilimo 2025/2026 NFRA kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imejipanga kuhakikisha wanatoa elimu kwa wakulima kuhusu mambo muhimu ya kuzingatia ikiwemo matumizi ya mbegu bora,kufuata kanuni kuanzia hatua za awali za kupanda hadi wakati wa mavuno.
Kwa mujibu wa Kahere,hatua hiyo itawasaidia wakulima kupata mahindi yenye ubora yanakayokidhi viwango ili kuepuka hasara,kuingia gharama kubwa kwa ajili ya kusafisha na kupoteza muda mwingi kwenye vituo vya ununuzi.
Amewataka wakulima,kuzingatia na kufuata maelekezo ya maafisa ugani na wataalam wengine wa kilimo wakati huu wanapoanza maandalizi ya msimu mpya wa kilimo ili waweze kupata mavuno mengi yatakayokubalika sokoni.
“Wakulima wasisite wala kuogopa kuwatumia maafisa ugani waliopo kwenye maeneo yao kwa ajili ya kupata ushauri wa kilimo cha kisasa badala ya kuendelea kulima kwa mazoea”alisisitiza Kahere.
Rais Samia Suluhu Hassan akiwa katika ziara ya siku saba mkoani Ruvuma,aliwapongeza wakulima kwa juhudi kubwa wanazofanya katika kuzalisha mazao kwa wingi na kuifanya Tanzania kuwa na usalama na uhakika wa chakula.
Aliwataka wakulima kuepuka kuuza kwa bei za walanguzi ya Sh.300, badala yake kuhakikisha wanauza mahindi yao kwa bei elekezi iliyotangazwa na Serikali ambayo ni Sh.700 kwa kilo moja.