Na Prisca Libaga Arusha
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) tarehe 10.12.2024  imeshiriki kufungua Mkutano wa Mashauriano ya Umoja wa Afrika Juu ya Muunganiko wa Mataifa Katika Kupunguza Uhitaji wa Dawa za Kulevya “_African Union-Global Coalition Continental Consultation on Drug Demand Reduction_” uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Mount Meru jijini Arusha.
Mkutano huo utafanyika kwa muda wa Siku Nne kuanzia tarehe 10 hadi 13 Disemba 2024. Tanzania ndo nchi mwenyeji, nchi zaidi ya 30 ambazo ni wanachama wa Jumuiya ya Umoja wa Afrika zimeshiriki katika Mkutano huo.  Pia kulikuwa na Wawakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusiana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC). Lengo la mkutano ilikuwa ni kuunganisha nguvu kwa pamoja katika kuimarisha utoaji wa elimu sahihi pamoja na upanuzi wa huduma za tiba na utengamao barani Afrika.
Mgeni rasmi wa Mkutano huo alikuwa ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama. Mgeni rasmi alielezea dhamira ya Nchi ya Tanzania katika mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya katika kupunguza uhitaji wa dawa za kulevya na kuwaunganisha waraibu na huduma za matibabu na utengamao.
Mhe. Ummmy Nderiananga alielezea mafanikio ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) katika kupunguza upatikanaji wa dawa za kulevya, kutoa elimu katika makundi mbalimbali na kupanua huduma za matibabu na utengamao kwa waraibu wa dawa za kulevya nchini. Pia alieleza kuwa DCEA imefanikiwa kufungua Kituo cha Utoaji Huduma (Call Centre) ambapo wananchi wanaweza kupiga simu bure na kutoa taarifa za wahalifu wa dawa za kulevya muda wowote.
Umoja huo umempongea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa mafanikio makubwa aliyoyapata katika juhudi zake za dhati juu mapambano dhidi ya matumizi pamoja usafirishaji haramu wa dawa za kulevya nchini Tanzania.