Na. Coletha Charles, DODOMA
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kuimarisha juhudi za kutunza mazingira kwa kupanda miti ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kuimarisha mazingira.
Senyamule alizungumza hayo leo tarehe 9 Desemba, 2024 kwenye makutano ya barabara ya mzungu Makutupora katika kuazimisha miaka 63 ya uhuru wa Tanzania Bara, wenye kaulimbiu ya Uongozi Madhubuti na Ushirikishwaji kwa wananchi, ni msingi wa maendeleo yetu.
Alisema kuwa kila mwananchi anawajibu wa kuchangia katika juhudi za uhifadhi wa mazingira kwa kuhakikisha wanapanda miti katika maeneo yao kulingana na uhitaji wa kuwa na Dodoma ya kijani kila mahali. “Leo tumeanza kupanda miti katika barabara ya mzunguko. Kazi hii ni nzuri na uzuri wake ili ukamilike, tukija mwaka kesho tunaanza kuvuna maembe maana nasikia miti ya sasahivi haichelewi kubeba na hapo tutakuwa tumeona vizuri sura halisi ya mradi wa kupiganisha kijani. Lakini tunayo matumaini kupitia mradi huu Jiji la Dodoma linaenda kufanya mabadiliko makubwa katika sura yake ya ukijani wa jiji” alisema Senyamule.
Mkuu wa mkoa pia alitoa wito kwa viongozi wa mitaa na mashirika ya kijamii kushirikiana katika zoezi hii, ili kuhakikisha miti inayopandwa inatunzwa na kukua ili kuleta mabadiliko chanya katika mazingira ya Dodoma, na hivyo, kuboresha maisha ya wananchi. “Lakini nisisitize wilaya na halmashauri zote kipindi hiki cha mvua kimeanza, kampeni yetu ya kijanisha kila mahali tunaijua, kampeni na maelekezo ya Mheshimiwa Rais ya kupanda miti 1,5000,000 kila halmashauri tunaijua, ni wakati sasa wa kila mtu kuchukua hatua, kuanza kupanda miti. Bahati nzuri sana tuwashukuru TFS, kwa kuanzia wameshaanza kutuoteshea tena wanatoa bure” alisema Senyamule.
Hata hivyo, alitoa shime kwa kamati za maafa za wilaya zote za Mkoa wa Dodoma kuendelea kufuatilia mabadiliko ya hali ya hewa na kuchukua hatua za athari za mvua kwa kutoa taarifa mapema.
Mtendaji Mkuu wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo, alisema wataanza kutoa utaalamu nchi nzima wa kupanda miti ili kuwa na misitu ya mijini kwa kuwezesha miti mbalimbali na kuhakikisha kunakuwa na Tanzania ya kijani. “Miaka takribani sita tulisaini makubaliano kati ya TFS na Halmashauri ya Jiji la Dodoma ya kuwa TFS tunawajibu wa kuhakikisha tunatoa msaada wa vifaa na miche ya miti. Lakini pia miaka 63 ya Uhuru wa nchi yetu, inayo wajibu wa kulinda mazingira yetu na tunadhamana ya kupanda miti” alisema Prof. Silayo.
Tanzania bara ilipata uhuru wake tarehe 9 Desemba 1961, baada ya miaka mingi ya harakati za kisiasa na mapambano dhidi ya ukoloni. Wakati huo, viongozi kama vile Hayati Mwl. Julius Kambalage Nyerere waliongoza juhudi za kuleta mabadiliko na kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kujitawala, maadhimisho ya siku hii yanatoa fursa ya kukumbuka safari ya nchi na kutathmini mchango wa kila mmoja katika kutunza na kuimarisha rasilimali, ikiwa ni pamoja na mazingira.