TAARIFA KWA UMMA
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa kwa kuhakikisha linabaini, kuzuia na kupambana na uhalifu ili kuwafanya wananchi waendelee na shughuli zao za kujipatia kipato halali bila usumbufu wala matishio yoyote.
Katika kipindi cha mwezi Novemba, 2024 jumla ya watuhumiwa wa makosa 97 wa makosa ya mauaji, kujeruhi, kupatikana na dawa za kulevya, kuingia nchini bila kibali na kupatikana na silaha bila kibali walikamatwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya kutokana na oparesheni na misako.
Novemba 21, 2024 huko katika kizuizi cha Polisi [Police Check Point] kilichopo mpakani Kijiji cha Igawa wilaya ya Mbarali, Jeshi la Polisi liliwakamata Shamim Maxwell [37] na Itika Bugale [36] wote wakazi wa Uyole Jijini Mbeya wakiwa na dawa za kulevya aina ya Bhangi Kilogramu 33.5
Watuhumiwa walikamatwa wakiwa wanasafirisha bhangi hiyo wakitokea Uyole kuelekea Dar es Salaam wakiwa abiria kwenye Gari yenye namba za usajili T.792 EDR Zhongtong Bus mali ya kampuni ya Achimwene.
Watuhumiwa walitumia mbinu ya kuficha dawa hizo za kulevya kwenye mabegi mawili ambayo ndani yake yalikuwa na nguo na walibainika baada ya kufanyika ukaguzi.
Wakati huo huo, Novemba 21, 2024 huko katika kizuizi cha Polisi kilichopo mpakani Kijiji cha Igawa Wilaya ya Mbarali, katika ukaguzi wa magari, Jeshi la Polisi lilifanikiwa kumkamata Kondakta wa Basi la Abood aitwaye Erick Patrick Mathew [46] na Tingo wa Basi hilo aitwaye Stanslaus Medson Nyagawa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Bhangi zenye uzito wa kilogramu 20.
Watuhumiwa walikuwa wakisafirisha dawa hizo kwenye Basi la Abood lenye namba za usajili T.823 DXJ Youtong wakitokea Mkoa wa Songwe kuelekea Dar es Salaam ambapo walificha dawa hizo kwenye mifuko miwili mikubwa ya sandarusi.
Sambamba na hayo, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Askari wa TANAPA likiwa katika doria ndani ya hifadhi ya Taifa ya Ruaha, linamshikilia Adam Bandari Katani [58] mkazi wa Chunya kwa tuhuma za kupatikana na silaha aina ya Gobore bila kuwa na kibali cha kumiliki silaha hiyo.
Mtuhumiwa alikutwa na vipande 30 vya chuma ambavyo huvitumia kama risasi katika silaha hiyo, Unga wa baruti ukiwa kwenye kopo, Fataki 5 na vipande 7 vya nyama ya mnyama pori aina ya pimbi bila kuwa na kibali. Mtuhumiwa amekuwa akijihusisha na matukio ya uwindaji haramu ndani ya hifadhi ya taifa ya Ruaha.
Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na jitihada za kuzuia na kudhibiti ajali za barabarani ambapo kwa kipindi cha mwezi Novemba 2024 jumla ya makosa ya usalama barabarani 10,580 yalikamatwa kati yake magari yalikuwa 9,155 na pikipiki zilikuwa 1,425 ambapo magari yaliyokaguliwa yalikuwa 9,155.
Pia, katika kipindi hicho jumla ya madereva 02 walifungiwa leseni zao za udereva kutokana na makosa hatarishi kama vile mwendo kasi na kusababisha ajali za vifo. Kesi zilizofikishwa mahakamani zilikuwa 07 ambapo zote zilipata mafanikio baada ya madereva kukutwa na hatia na kutakiwa kulipa faini.
Mahakamani, jumla ya kesi zilizofikishwa mahakamani zilikuwa 242 kati ya hizo kesi 92 zilipata mafanikio na kesi 150 zipo katika hatua mbalimbali. Miongoni mwa kesi zilizopata mafanikio ni kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na hatia kwa kosa la kumbaka mwanafunzi.
Erick Lucas Simtengu [24] mkazi wa Kijiji cha Mbugani Wilayani Chunya amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Isenyela mwenye umri wa miaka 15 [Jina linahifadhiwa].
Hukumu hiyo imetolewa katika Mahakama ya Wilaya ya Chunya mbele ya Hakimu Mheshimiwa.James Mhanus Novemba 12, 2024 na Mwendesha Mashitaka wa Jeshi la Polisi Mkaguzi wa Polisi Kahiwa Mayanja ambapo mshitakiwa alitenda kosa hilo Julai 17, 2024 baada ya kumtorosha mhanga kutoka kwenye Bweni la Shule usiku na kumpeleka nyumbani kwake na kufanya naye mapenzi hadi asubuhi.
Vile vile, Modrick Elias Mwakibete [21] mkazi wa Uyole Jijini Mbeya amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kubaka alilolifanya kwa mtu mzima [Jina linahifadhiwa] baada ya kumtishia kumchoma kwa kisu na kisha kutimiza adhima yake.
Hukumu hiyo imetolewa katika Mahakama ya Wilaya ya Kyela mbele ya Hakimu Mheshimiwa Paul Barnabas na Mwendesha Mashitaka wa Polisi Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Bihemo Dawa Mayengela ambapo mshitakiwa alitenda kosa hilo Machi 23, 2024 baada ya kuwasiliana na kukutana na mhanga kisha kubadilisha mad ana kumlazimisha wafanye mapenzi huku akimtishia kumchoma kisu ambacho alikuwa nacho.
Hukumu hizo zimetolewa kwa mujibu wa kifungu cha 130 kifungu kidogo cha kwanza na cha pili (b) na kifungu cha 131 kifungu kidogo cha kwanza vyote vya sheria ya kanuni ya adhabu.
Pia, Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya imewahukumu kunyongwa hadi kufa Emanuel Patson Mwesya [24] na David Saimon Mwalindu [25] wote wakazi wa Mji wa Tunduma Mkoa wa Songwe baada ya kukutwa na hatia kwa kosa la mauaji walilolifanya kwa kumuua Lufingo Asumwisye [37] aliyekuwa Mkazi wa Kijiji cha Bitimanyanga Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya.
Hukumu imetolewa na Mheshimiwa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Aisha Pinda na Mwendesha Mashitaka wa Serikali Veneranda Masai Novemba 19, 2024 kwa mujibu wa vifungu namba 196 na 197 vyote vya sheria ya kanuni ya adhabu, washitakiwa walitenda kosa hilo Januari 01, 2022 baada ya kumvizia Lufingo Asumwisye akiwa shambani kwake kisha kumuua kwa kumkata kwa kitu chenye ncha kali kichwani kisha kumuibia Pikipiki yake.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa rai kwa baadhi ya wananchi wanaendelea kufanya vitendo vya uhalifu kuacha kwani uhalifu haulipi na badala yake watafute shughuli nyingine za kufanya ili kujipatia kipato halali. Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa wazazi na walezi kuimarisha ulinzi wa mtoto hasa katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za mwisho na mwanzo wa mwaka ili kuwaepusha na hatari ikiwemo vitendo vya ukatili na unyanyasaji.
Imetolewa na:
Benjamin Kuzaga – SACP
Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya
www.polisi.go.tz www.twitters.com ‘tanpol’ www.facebook.com’PolisiTanzania’ www.instagram.com’polisi.tanzania’