Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Tanga – Wizara ya Madini imesema itaongeza juhudi katika kuhakikisha kuwa Bodi ya Wanajiolojia Tanzania (TGS) inaundwa kwa haraka ili kuwawezesha wataalamu hao kuungana na kuchangia mabadiliko chanya katika sekta ya madini.
Hayo yalibainishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wataalamu wa Wanajiolojia, mkutano wa siku mbili uliofanyika jijini Tanga na kushirikisha wataalamu kutoka ndani na nje ya nchi.
Mbibo alieleza kuwa hatua hiyo inatokana na wito ulioitolewa na Rais wa Jumuiya ya Wanajiolojia Tanzania, Dkt. Elisante Mshiu, ambaye alisisitiza kuwa ukosefu wa bodi hiyo unaweza kuzuia juhudi za sekta ya madini kufikia malengo ya maono ya 2030.
“Wizara ya Madini imeendelea kutoa mchango muhimu kwa kutumia utaalamu wa wanajiosayansi katika tafiti za kubaini uwepo wa madini nchini, kupitia maono ya Vision 2030. Madini ni maisha, ni utajiri na ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya taifa letu,” alisema Mbibo.
Naibu Katibu Mkuu aliongeza kuwa wanajiosayansi wanachangia kwa kutumia teknolojia ya kisasa, ikiwemo tafiti za jiofizikia, ambazo ni muhimu kwa kutambua tabia za miamba na kubaini aina mbalimbali za madini nchini.
Kwa upande wake, Rais wa Jumuiya ya Wanajiolojia Tanzania, Dkt. Elisante Mshiu, alisema kuwa mkutano huo unalenga kujadili mabadiliko katika sekta ya nishati, ikiwa ni pamoja na mpito kutoka kwa nishati chafuzi kwenda kwenye nishati salama, ambayo ni sehemu ya malengo ya serikali.
Dkt. Mshiu alisisitiza kuwa bila kuwa na Bodi ya Usajili ya Wanajiosayansi, maono ya 2030 yanaweza kukutana na changamoto kubwa. Alitoa wito kwa serikali kuhakikisha kuwa juhudi za uundwaji wa bodi hiyo zinafanyika kwa haraka ili kuendana na kasi ya maendeleo ya nchi.
“Kupitia Wizara ya Madini, juhudi kubwa zinafanyika na hatua hizo ziko karibu kumalizika. Tumesisitiza umuhimu wa kuharakisha mchakato huu ili kuhakikisha maendeleo yanakua kwa kasi inayohitajika,” alisisitiza Rais Mshiu.
Wanajiosayansi kutoka ndani na nje ya Tanzania walikusanyika jijini Tanga kwa mkutano wa TGS 2024, ambao unalenga kupeana taarifa za kitaalamu, kubadilishana uzoefu, na kujadili masuala yanayohusu utafutaji na uendeshaji wa rasilimali za madini, mafuta, gesi asilia, maji, na joto la ardhi.