Na. Lusungu Helela- Dodoma
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amesema Wananchi walio wengi wamekuwa wakitumia mitandao ya Kijamii kufikisha malalamiko yao kwenye Taasisi za Serikali kutokana na baadhi ya Watumishi wa Umma kuvujisha siri za wateja wao pindi wananchi hao wanapotumia mifumo rasmi kutoa mrejesho
Amesema vitendo hivyo vimekuwa vikiwakatisha tamaa Wananchi wenye nia njema ya kuona Serikali inakuwa kinara wa kutoa huduma bora kwa wananchi wake.
Bw. Daudi ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo maalum ya siku tatu kwa Maafisa Mrejesho kuhusu uendeshaji wa mfumo wa e-Mrejesho katika Ofisi za Umma
Amewataka Maafisa hao kutunza siri za wateja wao ili kuwafanya Wananchi kuwa huru kuwasilisha changamoto zinazowakabili wakati wowote na mahali popote pasipo kulazimika kutumia mitandao ya kijamii
Bw. Daudi ameongeza kuwa Mfumo wa e-Mrejesho unampa fursa mwananchi kutuma malalamiko, pongezi pamoja na maulizo kwa Serikali mahali popote na wakati wowote.
Kufuatia hatua hiyo Bw. Daudi amewataka Maafisa hao mara baada ya kurudi katika vituo vyao vya kazi wakahakikishe wanakuwa waadilifu na wenye kutunza siri za ofisi na za wateja wao ili kuwafanya wananchi kuwasilisha malalamiko yao kwenye njia rasmi
Aidha, Bw. Daudi amewataka Maafisa hao wakaimarishe Madawati au Ofisi za Mrejesho zilizopo katika Taasisi zao ili kufanikisha ushughulikiaji mrejesho kwa ufanisi na kwa wakati katika Ofisi za Umma kwa vile wameaminiwa kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Usimamzi wa Utawala Bora kutoka USAID/PS3+ awamu ya pili Dkt. Emmanuel Malangalila amesema wataendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha mfumo huo unatumika ipasavyo katika Serikali za Mitaa ambako ndiko kuna malalamiko makubwa kutoka kwa wananchi .
Mafunzo haya yanalenga kuona huduma zinazotolewa na Serikali zinafurahiwa na wananchi wote bila kujali rangi, kabila, mahali au hali yao ya kiuchumi waliyonayo amesisitiza Dkt. Malangalila
Hivi karibuni Tanzania ilipewa tuzo ya Kimataifa ya ubunifu wa mfumo ya kidijitali wa Mrejesho (e-Mrejesho) nchini Korea Kusini na Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) wakati wa Mkutano wa Umoja wa Jukwaa la Umoja wa Mataifa la Tuzo za Utumishi wa Umma (2024 UN Public Service Awards (UNPSF) kutokana na umadhubuti wake.