Na Ashrack Miraji Same Kilimanjaro
Watu 439 Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro katika kipindi cha miezi 11 kuanzia mwezi Januari hadi Novemba 2024 wamekutwa na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) kati ya watu 21,876 waliojitokeza kwenye Vituo vya Afya kupima ugonjwa huo.
Desemba 01 kila mwaka Dunia huadhimisha siki ya UKIMWI, lengo likiwa ni kuwakumbuka waliopoteza maisha kutokana na ungonjwa huo ili kujifunza na kuchukua hatua stahiki za kujikinga na maambukizi mapya yanayoweza kuchukua uhai wa watu wengine. Kwa mwaka huu wa 2024 maadhimisho haya yamepambwa na kaulimbiu isemayo “CHAGUA NJIA SAHIHI TOKOMEZA UKIMWI”.
Wilayani Same Maadhimisho hayo yamefanyika katika viwanja vya Kwasa Kwasa Kata ya Kisima ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya hiyo kasilda Mgeni, Maadhimisho hayo yameambatana na utoaji huduma za Afya kwa wananchi wa Same ikiwemo upimaji wa Virusi vya UKIMWI yaani VVU.
Akizungumza kwenye maadhimisho DC Kasilda amesisitiza wakazi wa Same kuendelea kuunga mkono jitihada za Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha wanapiga vita ugonjwa huo ili usiendelee kuathiri jamii.
Aidha ameelekeza Halmashauri ya Same kuendelea kushirikiana na Taasisi na Mashirika yasiyo ya kiserikali kutoa elimu juu ya UKIMWI kwa vijana ili kuweza kuwa na kizazi bora na chenye uelewa mzuri wa namna ya kujikinga na janga hili.