Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyamagana, akizungumza na wana CCM wakiwemo wananchi wa wilaya leo, katika mkutano wa kuwapongeza wenyeviti na wajumbe wa serikali za mitaa kwa ushindi.
NA BALTAZAR MASHAKA,MWANZA
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza,Jamal Abdul ‘Babu’,amesema ushindi walioupata wagombea wa Chama katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024,umetokana na kazi nzuri ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi 2020-2025.
Akizungumza leo katika mkutano wa kuwapongeza wenyeviti na wajumbe wa serikali za mitaa walioshinda katika Wilaya ya Nyamagana,amesema CCM imepata ushindi kwa kazi nzuri ya kuleta maendeleo iliyofanywa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.
“Tumepata ushindi kwa kazi zilizofanyika za maendeleo,nendeni mkawatumikie wananchi bila kujali itikadi zao za vyama,maendeleo hayana vyama na tukazingatiye 4R (Maridhiano,Ustahimilivu,Mageuzi na Kujenga) za Mh.Rais Dk.Samia,”amesema Babu.
Amesema ushindi huo usiwafanye wana CCM na viongozi kubweteka wakawahudumie wananchi kwa sababu wao ndio watakaoiweka CCM katika eneo salama kulekea uchaguzi mkuu mwakani.
Babu amesema Rais Samia amefanya kazi kubwa ya kutekeleza ilani ya CCM na kuleta maendeleo ya kupigiwa mfano likiwemo Daraja la JPM ambalo wakati anaingia madarakani lilikuwa asilimia zaidi ya 20,sasa limefikia asilimia 98,soko la kisasa la Jiji,Meli ya MV Mwanza na reli ya SGR,vituo vya afya zaidi ya 300 na zahanati zaidi ya 900 zimejengwa.
Mjumbe huyo wa NEC pia,amewapongeza viongozi wa Chama na Serikali ngazi ya mkoa,wilaya, wanachama na wananchi kwa kazi kubwa iliyowezesha CCM kushinda katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024,katika vitongoji zaidi ya 3000 na vijiji 545,jijini Mwanza ikishinda mitaa 172 kati ya 175.
“Wakati kampeni zinaanza tuliomba ridhaa kwa wananchi tukiomba kura,kama haitoshi CCM imevuna wanachama wengi na kukifanya kiendelee kuwa bora zaidi,pokeeni salaam kutoka kwa mlezi wetu Katibu Mkuu,Balozi Dkt.Emmanuel Nchimbi anawasilimia pia anawapongeza kwa ushindi,”alisema.
Pia,Babu amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwezesha ushindi huo wa CCM,viongozi wa dini kwa kuendelea kukiombea Chama Cha Mapinduzi na kukishauri.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyamagana,Peter Begga katika mkutano huo,amesema vyama vya upinzani vilikwenda kunadi sera za CCM zaidi huku wakihoji wananchi itawafanyia nini, lakini wananchi walielewa.
“Viongozi wa vyama vya upinzani kazi yao ilikuwa ni kutukana na viongozi wa CCM na Serikali,walikwenda kunadi sera za CCM kuwa itawanyia nini wananchi,kwa ushindi huu 2025 tunakwenda kushinda Urais,ubunge na udiwani kwa kishindo,hizi zilikuwa mvua za rasharasha,”amesema.
Begga ameeleza ushindi wa CCM unawategemea wenyeviti wa Serikali za Mitaa,nafasi walizopata ni mali ya Chama ambacho kiliingia mtaani kuomba kura,hivyo wakawatumie wananchi wakishirikiana na wajumbe wao badala ya kufanya kazi peke yao.
“Wananchi wa Nyamagana wamejitoa na kuwapa kura zao, nendeni mkafanye kazi ya kuwatumikia,tusisikie mwananchi anaombwa hata sh.10 ya kuandikiwa barua ya utambulisho,atakayebainika atafikishwa kwenye kamti ya maadili,”amesema na kuongeza kuwa wataendelea kuwapa semina ili kazi iwe rahisi 2025.
Awali Katibu wa CCM Nyamagana, George Nakei amesema ushindi wa wenyeviti wa mitaa na wajumbe wao haukuja kwa bahati mbaya bali uliandaliwa, waliwashukuru wananchi wa wilaya hiyo kwa kuendelea kuiamini CCM na kuwapigia kura wagombdea wake.