Uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) ukiongozwa na Mkuu wa Chuo, Prof. Eliamani Sedoyeka wamefanya ziara nchini Uingereza kwa ajili ya kujifunza na kuangalia njia mbalimbali za kuboresha huduma za ujifunzaji na ufundishaji.
Katika ziara hiyo Uongozi wa IAA umetembelea ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza na kukutana na Mheshimiwa Balozi Mbelwa Brighton Kairuki.
Mhe. Balozi amekipongeza Chuo kwa juhudi zake katika kuboresha elimu na pia amejadiliana na viongozi juu ya fursa mbalimbali zilizopo nchini uingereza katika sekta ya elimu na nyinginezo.
Aidha , Novemba 19, 2024 Mkuu wa Chuo Prof. Eliamani Sedoyeka na timu yake wametembelea ARU university (Anglia Ruskin University) mjini Cambrigde ambapo pamoja na mambo mengine mengi wamejadili masuala mbalimbali ya kitaaluma, tafiti na ushauri. Lengo ikiwa ni kujifunza na kubadilishana uzoefu kwa lengo la kuendelea kuboresha ufundishaji, ujifunzaji na huduma mbalimbali zinazotolewa na Chuo.
Prof. Sedoyeka ameeleza kuwa, ajenda ya serikali ni kuhakikisha Taasisi za Elimu ya Juu zinatoa huduma kwa hadhi ya Kimataifa na IAA kama Taasisi ya Umma tumejipanga kuhakikisha kuwa tunatoa huduma katika ubora wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuwa na mitaala inayokidhi viwango vya kimataifa, kuongeza udahili wa wanafunzi wa kimataifa na kuhakikisha wahitimu wetu wanakidhi soko la ajira la ndani na lile la kimataifa.
Katika ziara hiyo Chuo kinatarajia kutembelea vyuo vingine ikiwemo Oxford university, Nottingham University, commonwealth AI academy pamoja na kukutana na Watanzania (Diaspora) waishio Uingereza ambao ni wataalam katika sekta za fedha, uhasibu, uchumi, tehama na nyingine nyingi.