Mganga mfawidhi wa hospitali ya mkoa Mount Meru ,Dokta Ernest Martin akizungumza kwenye mahafali hayo mkoani Arusha.
Mkurugenzi wa Shirika la Help to Self Help ,Amani Golugwa akizungumza katika mahafali hayo mkoani Arusha leo
Happy Lazaro,Arusha .
Wahitimu wa kozi za mafunzo ya ufundi katika chuo cha ufundi Help to Self Help wametakiwa kuwa mabalozi wazuri wa mafunzo ya ufundi stadi na kuonyesha jamii umuhimu wa mafunzo hayo kwani yana mchango mkubwa katika.ujenzi wa uchumi.wa nchi yetu.
Hayo yamesemwa mkoani Arusha na Mganga mfawidhi wa hospitali ya mkoa Mount Meru ,Dokta Ernest Martin ambaye alimwakilisha Naibu waziri wa Afya ,Dokta Godwin Mollel katika mahafali ya 25 ya chuo hicho ambapo jumla ya wanafunzi 82 wamehitimu.
Amesema kuwa,elimu ya ufundi ina jukumu kubwa katika maendeleo ya Taifa letu,huku akiwataka kuendelea kujifunza na kuboresha ujuzi zaidi kwani dunia inabadilika kwa kasi na ni muhimu kubaki na hamasa ya kujifunza ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazoendana na maendeleo ya kiteknolojia na kijamii.
“Chuo hiki ni moja kati ya vyuo bora nchini vyenye uzoefu usio na.mashaka katika kutoa mafunzo ya ufundi stadi katika.fani mbalimbali inazotoa hivyo nawahimiza kuthamini mchango wa walimu wenu na wazazi ,kwani mmekuwa nguzo muhimu katika safari yenu ya elimu ya ufundi na mmekuwa kama mwongozo, mkionyesha njia na kuwapa mwongozo wa kufanikiwa.”amesema .
Amesema kuwa, mapitio ya sera ya elimu ya hivi karibuni yameelekeza elimu ya amali kuwa sehemu ya elimu ya lazima kato ya kidato cha kwanza hadi cha nne ,ambapo kwenye hili serikali imekusudia kusimamia na kuhakikisha mafunzo haya yanafanyika mashuleni kivitendo na sio nadharia kwa sababu wanatambua mafunzo ya ufundi stadi ni msingi muhimu wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa maana inaongeza nguvu kazi katika uzalishaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Help to Self Help ,Amani Golugwa amesema kuwa ,chuo hicho kimekuwa kikitoa wanafunzi mahiri na waliobobea kwenye kozi mbalimbali ambao wanakuwa tayari kuajirika pindi wanapohitimu masomo yao.
Golugwa amewataka wanafunzi hao kujibidiisha sana kwenye teknolojia katika kuyajua mambo na sio kuogopa huku wakienda sambamba na mabadiliko ya teknolojia yaliyopo hivi sasa .
“Tunawaomba sana wekeni bidii katika kujiridhisha kwenye huduma mnazotoa hakikisheni mnatoa huduma shindani na ijulikane ni vijana waliopikwa vizuri kutoka chuo hiki na mhakikishe mnakitangaza vizuri chuo hiki popote mtakapokuwa kutokana na umahiri mkubwa tulionao wa kutoa vijana waliobobea katika.fani mbalimbali kwa vitendo.”amesema .
Aidha amesema kuwa,chuo hicho kinakabiliwa na upungufu wa hosteli ambapo ambapo wameshaandaa michoro ya kujenga hosteli kubwa ambayo itaweza kuchukua wanafunzi zaidi ya 250 wa kike na wa kiume.
“Mradi huu wa ujenzi wa hosteli tumetamani sana tuufanye kwa ubia na serikali kupitia utaratibu wa “Public ,Private ,Partnership -PPP,ambapo wameomba serikali uwashike mkono katika kusaidia kurudi hilo.
Kwa upande wake Mkuu wa chuo hicho ,Ester Mwasape amesema kuwa,chuo hicho kinatoa mafunzo ya ufundi stadi kwa ufanisi katika vitendo kwa kanda ya kaskazini,ambapo kitendo hicho kinawezesha wanafunzi kumudu kazi ambazo wanajifunza kupitia fani zao.
Amesema kuwa, kwa mwaka 2024 chuo hicho kimeongeza fani mbili za umeme wa magari na uongozaji watalii ambazo bado hazina karakana za kudumu za wanafunzi kuweza kujifunza ili kujenga ujuzi bora kwenye fani ya umeme wa magari na vifaa vya kisasa kwa fani ya kuongoza watalii,karakana hizo zitaongeza ufanisi na kupanua wigo wa elimu kwa jamii nzima ya Arusha na Tanzania .