*******************************
KAMATI ya Utendaji ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA) , inawahimiza wanachama wake ambao wana nia ya kushiriki Mkutano Mkuu Maalum wa chama hicho kuhakikisha wanathibitisha kwa maandishi ili waweze kuhudhuria mkutano huo.
Hatua hiyo inatokana na mwitikio mdogo wa waliothibitisha kushiriki, hivyo kufanya maandalizi mengine ya mkutano huo kushindwa kufanyika vizuri.
Kwa mazingira hayo mwisho ya kuthibitisha kushiriki itakuwa Jumatatu Januari 13 mwaka huu, na mkutano huo sasa utafanyika Jumapili Januari 19 na hakutakuwa na muda wa ziada kwa watakaoshindwa kuthibitisha.
Lengo la mkutano huo ni kujadili masuala mbalimbali ya chama, ambapo pia utapokea taarifa kutoka Kamati ya Marekebisho ya Katiba iliyoundwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na pia utapokea mapendekezo kutoka Kamati ya Utendaji ya TASWA inayomaliza muda wake.
Watakaohudhuria Mkutano Mkuu Maalum ni wanachama wote walio katika leja baada ya kushiriki uchaguzi wowote wa TASWA kuanzia mwaka 2004, 2007, 2010, 2014 na wanachama wapya wote walioingia kuanzia mwaka 2015 hadi Juni mwaka jana.
Kwa mazingira hayo ili mkutano ufanyike kwa ufanisi ni vyema yeyote mwenye nia ya kushiriki athibitishe kwa maandishi akitaja jina lake na chombo na kutuma kwa email: [email protected] au [email protected] au [email protected], ili taratibu nyingine ziendele.