Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe David Kihenzile akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa jina jipya la kampuni ya meli TASHICO Jijini Mwanza
Baadhi ya wadau walioshiriki katika uzinduzi wa jina jipya la Kampuni ya Meli TASHICO Jijini Mwanza
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya TASHICO akizungumza kwenye uzinduzi wa jina jipya la kampuni ya meli
Na Hellen Mtereko,Mwanza
Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) imefanya mabadiliko ya jina la kampuni hiyo ambapo kwa sasa inaitwa Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) ikiwa ni sehemu ya kuongeza wigo katika huduma za usafiri wa majini.
Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa jina hilo jipya na nembo mpya ya kampuni hiyo uliofanyika Leo Jumatatu Novemba 18, 2024 katika Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, Mkurugenzi Mtendaji wa TASHICO, Eric Hamissi alisema mabadiliko hayo ni sehemu ya kupanua wigo wa utoaji huduma sanjari na kujikita katika upanuzi wa biashara kwenye maeneo ya maziwa makuu na Bahari ya Hindi.
Alisema lengo lao ni kuwa na meli nyingi zikiwemo za kubeba mizigo huku akieleza matarajio ya kuwa na meli katika Bahari ya Hindi.
“Tunatarajia kuwa na meli zisizopungua nne katika Bahari ya Hindi ifikapo mwaka 2030 lengo ni kuendeleza sekta hii ya uchukuzi ili iweze kuleta tija kwenye Taifa”, alisema Hamissi
Kwaupande wake Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile ameielekeza menejimenti ya TASHICO kuongeza ubunifu katika eneo la huduma kwa wateja hususani kwa huduma za abiria na mizigo
Pia amewaasa kusimamia kwa karibu wakandarasi ili miradi yote inayotekelezwa kwenye ukarabati na ujenzi wa meli ikamilike kwa wakati na kwakuzingatia thamani ya fedha.
Kihenzile alisema katika kipindi cha miaka mitatu Serikali imetoa tillioni 1.2 kwa ajili ya kuboresha miradi ya meli kwenye maziwa makuu.
Awali akitoa salam kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda, Katibu Tawala wa mkoa huo Elikana Balandya alisema miundo mbinu ya usafiri na usafirishaji ikiwa imara inasaidia kuboresha uchumi wa wananchi hivyo akishukuru Serikali kwanamna inavyoendelea kuboresha sekta ya uchukuzi.