Viongozi wametakiwa kuzingatia maadili ili kuweza kuwatumikia vyema wananchi, wana chama wa chama cha mapinduzi na jamii kwa ujumla
Rai hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya ya Ilemela ambae pia ni mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa na kamati ya siasa wilayani humo Mhe Hasan Elias Masala wakati akizungumza na mabalozi wa chama hicho kuwaelekeza wajibu wao kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024 katika ukumbi wa The Breeze kata ya Kiseke ambapo amewataka viongozi waliochaguliwa kuwania nafasi za uenyekiti wa serikali za mitaa na wajumbe wa kamati za mtaa kuzingatia maadili na miiko ya uongozi ili kuondoa taharuki katika jamii pamoja na kusaidia chama kupata ushindi kwa urahisi
‘.. Neno tunalotakiwa kulipigia mstari katika tafsiri sahihi ya maadili ni kujiheshimu, Ukilewa sana utakuwa umeshatoka nje ya maadili sababu utafanya vitu vya ajabu katika jamii, Kwa nafasi yako kama kiongozi hautakiwi kufanya vitu vya ajabu sababu wewe ni kioo katika jamii ..’ Alisema
Aidha Mhe Masala amewataka wanachama wa CCM waliogombea nafasi za uongozi katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na kushindwa kuteuliwa kuacha mara moja usaliti na undumilakwili na kwamba chama hakiwavumilia ikiwemo kuwachukulia hatua kali hata kuwafukuza uanachama kwa watakaobainika kukisaliti katika chaguzi zinazoendelea
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Ukerewe Mhe Christopher Emily Ngubiagai amewapongeza wananchi wa wilaya ya Ilemela kwa kupata bahati ya kuwa na viongozi wazuri wanaojali watu wanaowaongoza na wenye uwezo wa kutatua kero na changamoto zao huku akiongeza kuwa mfumo wa vyama vingi vya siasa lengo lake ni kuongeza kasi ya maendeleo ya nchi, upinzani usio wa kiadui na upinzani unaoleta chachu katika maendeleo ya nchi tofauti na wanavyotafsiri watu wasiotakia mema nchi na wavunjifu wa amani
Nae katibu wa CCM wilaya ya Ilemela Ndugu Hasan Milanga amempongeza mbunge Dkt Angeline Mabula kwa kujitoa kwake katika kukijenga chama na kukisaidia kila inapohitajika ili malengo yanayokusudiwa yaweze kutekelezeka huku akiwaasa viongozi wengine kuiga mfano huo
Akihimitisha Mbunge wa Jimbo la Ilemela na mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM Taifa (MNEC) Mhe Dkt Angeline Mabula licha ya kuwapongeza viongozi wa CCM wilaya ya Ilemela kwa kufanya ziara ya kuwaweka pamoja wanachama katika matawi baada ya uchaguzi amewataka viongozi na wanachama kuendelea kuwa pamoja, kushikamana na kuunganisha nguvu kuhakikisha CCM inaenda kushinda uchaguzi wa serikali za mitaa 2024