Fundi anayesimamia mradi wa maji katika kijiji cha Kiranjeranje Said Mayogo akionyesha kisima cha maji kilichochimbwa tangu mwaka 1954.
Nyumba ya mashine(Pump House) inayosukuma maji kutoka kwenye kisima kwenda kwenye makazi ya watu katika kijiji cha Kiranjeranje wilayani Kilwa.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Kiranjeranje wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, wakichota maji kutoka kwenye moja ya kituo cha kuchotea maji kama walivyokutwa na Mpoga picha wetu.
Na Mwandishi wetu,
Kiranje ranje
BAADHI ya wakazi wa kijiji cha Kiranjeranje kata ya Kiranjeranje wilaya ya Kilwa mkoani Lindi,wameiomba Serikali kupitia wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)kuboresha huduma ya maji kwa kutafuta vyanzo vyenye maji baridi.
Wamesema,kwa sasa wanautumia maji machungu yenye radha ya chumvi hasa baada ya Ruwasa kufanya ukarabati wa kisima kilichochimbwa tngu mwaka 1954 kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji ambacho awali maji yake yalikuwa baridi.
Omari Bushir alisema,katika kijiji chao kuna kisima kikubwa chenye uwezo wa kuzalisha maji mengi,lakini maji yake yana asili ya chumvi,hivyo njia pekee ya kuepukana na adha hiyo ni Serikali kupitia Ruwasa kuhakikisha inatafuta chanzo kipya cha maji baridi.
“kwani Serikali kuwa na miradi miwili ya maji inayoingiza fedha kuna tatizo haya ndiyo maendeleo ya kweli,sisi wananchi wa kijiji hiki tunapata tabu kubwa kwa kutumia maji ya chumvi,tunaiomba sana Serikali yetu ya mama Samia kumaliza kero hii kwa kutafuta chanzo kingine cha maji baridi”alisema Bushir.
Alisema,maji wanayotumia ni machungu hayafai kuogea,kunywa,kufulia na kupikia chakula kama
vile maharage,kunde na mbaazi badala yake yanafaa kwa ajili ya kupikia mboga za majani na samaki.
Ameomba kujengwa tenki jipya lenye uwezo wa kuhifadhi maji mengi, badala ya kuendelea kutumia tenki la sasa ambalo halikidhi mahitaji ya idadi ya watu waliopo katika kijiji hicho.
Mkazi mwingine wa kijiji hicho Issa Hassan Sahara alisema,baadhi ya watu wanatumia gharama kubwa kununua maji ya chupa kwa ajili ya matumizi ya kila siku, jambo linalowasababishia umaskini mkubwa.
Alisema,zaidi ya asilimia 95 ya wakazi wa kijiji hicho ni wakulima hivyo hawana uwezo wa kupata fedha za kuwawezesha kumudu gharama za kununua maji,lakini njia pekee ni Serikali kutafuta chanzo kingine cha maji baridi ili waweze kuepuka kuingia gharama za kununua maji madukani hali inayowarudisha nyuma kiuchumi.
Fundi anayesimamia mradi huo Seleman Mayogo alisema,kijiji cha Kiranje ranje kuna kisima chenye uwezo wa kuzalisha lita 12,000 za maji kwa saa moja,lakini changamoto iliyopo ni sehemu ya kuhifadhia maji.
Kwa mujibu wa Mayogo, tenki lililopo lina uwezo wa kuhifadhi lita 45,000 na kwa siku wanalazimika kujaza mara tatu ili kutosheleza mahitaji ya maji kwa wakazi wa kijiji hicho wanaokadiriwa kufikia zaidi ya 13,000.
Alisema,kutokana na hali hiyo wanalazimika kutoa huduma ya maji kwa mgao ili maeneo mengi yapate huduma ya maji hiyo,lakini suluhisho la kudumu ni kujengewa tenki kubwa litakalokuwa na uwezo wa kuhifadhi maji mengi kwa wakati mmoja.
“Ruwasa tangu ilipoanzishwa mwaka 2019 imefanikiwa sana kuboresha miundombinu ya maji hasa kwa kusogeza huduma ya maji mitaani,lakini changamoto iliyopo ni tenki la kuhifadhia maji ambalo halina uwezo mkubwa wa kuhudumia kijiji hiki kutokana na idadi ya watu waliopo”alisema Mayogo.
Hata hivyo alisema,katika uendeshaji wa mradi huo changamoto kubwa wateja kuchelewa kulipa ankara za maji kwa wakati na wengine kulalamikia bili kuwa kubwa,hivyo ameiomba Serikali kuanza kuwafungia wateja mita za malipo kabla ya matumizi (Pre Paid) ambazo zitasaidia kumaliza malalamiko hayo.
Mayogo,amewashukuru wananchi wa kijiji Kiranje ranje kwa kutunza miundombinu ya maji inayojengwa na kuwataka kuendelea kushirikiana na Serikali yao kwa kulinda vyanzo vya maji na mradi huo kwa ujumla.