Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Katavi Christopher Nakua akimkabidhi mkuu wa mkoa wa Katavi fedha zilizorejeshwa kutoka kwa makarani
Fedha Tsh. 52,500,000/- zilizorejeshwa kutoka kwa makarani wa pamba wasio waaminifu
………………………
Na Mwandishi wetu Katavi
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Katavi imekabidhi kiasi cha shilingi milioni 52.5 kwa mkuu wa mkoa wa Katavi; fedha ambazo zimepatikana kutoka kwa makarani wa zao la pamba wa Chama cha Msingi Mpanda kati wasio waamifu walioandika majina feki na kisha kujilipa fedha hizo wao wenyewe
Bwana Christopher Nakua ni Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Katavi amesema kazi hiyo imefanyika kwa kipindi Januari hadi Desemba mwaka uliopita ambapo makarani hao walitumia majina hayo kujilipa
Aliongeza kuwa walifanya ufuatiliaji wa siri na kubaini mchezo mchafu unaofanywa na makarani hao
“Naamini fedha hizi tunazokabidhi leo zitafanya kazi kubwa ya maendeleo kwa vyovyote utakavyoona wewe mkuu wa mkoa” alisema Nakua
Akizungumza mara baada ya kupokea fedha hizo mkuu wa mkoa wa Katavi Juma Homera alisema hawatawafumbia macho watu wanaokiuka sheria
Aidha alisema fedha hizo zitatumika kutengeneza madawati 2080 ya shule za sekondari ili kupunguza tatizo la madawati katika shule hizo
Nao viongozi waliohudhuria katika hafla hiyo fupi ya makabidhiano wakiwemo wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama mkoa wameahidi kuendelea kuusimamia mkoa wa katavi katika kuhakikisha unasonga mbele
“Tutaendelea kushirikiana katika kufichua maovu na hii si tu kwa pamba bali pia na wahalifu wengine” alisema Kamanda wa Polisi mkoa Benjamin Kuzaga
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi Abdallah Malela aliahidi kusimamia utengenezaji wa madawati hayo
“Tuna upungufu wa madawati zaidi ya 6000 katika sekondari zetu, kwa hiyo madawati yatakayotengenezwa yatapunguza changamoto hiyo” alisema Malela