Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) leo Alhamisi, Januari 9, 2020 limetangaza matokeo ya mtihani wa upimaji darasa la nne, kidato cha pili na kidato cha nne.
Matokeo hayo yametangazwa na Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde amesema ufaulu katika mtihani wa upimaji wa darasa la nne umeongezeka kwa asilimia 26.21.
Jumla ya watahiniwa 1,531,120 kati ya wanafunzi 1,665, 863 wamepata alama A,B,C na D ikilinganishwa na wanafunzi 1,213, 132 waliofaulu mwaka 2018.
Katika mtihani wa upimaji kidato cha pili, wanafunzi 514,251 sawa na asilimia 90.04 kati ya wanafunzi 571,137 wamefanya vizuri katika mtihani huo na kuwawezesha kuingia kidato cha tatu.
Dk Msonde amesema mtihani wa kidato cha nne jumla ya watahiniwa 340,914 sawa na asilimia 80.65 ya watahiniwa 422,722 wameefaulu mitihani yao.
Watahiniwa hao ni sawa na ongezeko la asilimia 1.38 ikilinganishwa na watahiniwa 284,126 sawa na asilimia 79.27 waliofaulu mtihani huo mwaka 2018.