**************************************
NA EMMANUEL MBATILO
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni imeweza kudhibiti mianya ya Rushwa katika miradi ya maendeleo yenye thamani ya bilioni 12,217,537,000/= katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba 2019.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni, Bi.Theresia Mnjagira amesema kuwa katika kipindi hicho kubwa lilielekezwa katika kudhibiti vitendo vya Rushwa katika Uchaguzi wa Serikali za mitaa uliofanyika tarehe Oktoba 24 mwaka jana kwa kuhakikisha wananchi wanapata elimu kuhusu madhara ya rushwa katika uchaguzi na umuhimu wa kuchagua viongozi waadilifu kwa maendeleo ya taifa.
“Katika kutekeleza hilo TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni imekagua na kuhakiki miradi ya maendeleo tisa yenye thamani ya shilingi bilioni kumi na mbili milioni mia mbili na saba laki tano na thelethini na saba elfu (12,217,537,000/=) na kubaini kuwa kati ya miradi iliyokaguliwa mradi mmoja wenye thamani ya shilingi milioni themanini na sita na laki sita (86,600,000/=) una viashiria vya Rushwa”. Amesema Bi.Theresia.
Aidha Bi.Theresia amesema kuwa TAKUKURU katika Mkoa huo imechukua hatua ya kuanzisha uchunguzi kwa mradi mmoja uliobainika kuwepo ukiukaji wa taratibu kwa lengo la kujua sababu za ukiukwaji huo pale itakapothibitika kuwa vitendo vya rushwa vimetendeka hatua stahiki zitachukuliwa.
Pamoja na hayo Bi.Theresia ofisi ya TAKUKURU katika mkoa huo inatarajia kumfikisha mahakamani mtumishi wa Kinondoni Football Association (KIFA) kwa kosa la kuomba rushwa ya shilingi laki tano na kupokea shilingi laki tatu na thelathini.
“Ilidaiwa kuwa mnamo tarehe 18/11/209 mtuhumiwa aliomba rushwa ya shilingi 500,000/= ili aipitishe timu ya Ndumbwi kucheza ligi daraja la tatu kinyume cha utaratibu na sheria”. Ameeleza Bi.Theresia.