Na Mwandishi Wetu- Kigoma
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Peter Serukamba amesema suala la Afya za Watanzania sio suala la kufanyia siasa.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni ya Uhamasishaji wa wananchi kujiunga na mpango wa vifurushi vipya vya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya mkoani Kigoma, amesema kuwa mafanikio ya mwananchi ni kuwa na uhakika wa kupata matibabu kupitia bima ya Afya.
“Mwananchi anapokuwa na uhakika wa matibabu hapo ndipo ana mafanikio maana ataweza kushiriki shughuli za maendeleo. Ukiona mwanasiasa anapotosha suala la vifurushi huyo ni mwanasiasa uchwara maana afya si ya kufanyia siasa,” alisema Mhe. Serukamba.
Kutokana na hilo amewaomba wananchi mkoani Kigoma kutosikiliza upotoshaji na badala yake wachangamkie mpango huu ambao umelenga kumkomboa mwananchi.
“Mhe. Rais ametupunguzia sana mzigo, sasa watoto wanasoma bure hivyo kwa suala hili la Afya tuhakikishe na sisi tunajiunga na bima ya Afya,” alisema
Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF, Mama Anne Makinda amesema kuwa katika kipindi hiki watumishi wa Mfuko wataanza kupita majumbani na maofisini kwa lengo la kUtoa elimu ya masuala ya bima ya afya ili wananchi wachukue maamuzi ya kujiunga.
“Mhe. Rais halali na ndio maana amefanikiwa kufanya mambo makubwa hivyo na sisi wananchi tujitume na kutimiza wajibu wetu hasa wa kuhakikisha tunakuwa na uhakika wa huduma za matibabu” alisema Mama Makinda.
Akizindua mpango huo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga aliweka wazo kuwa ili mtu awe na uhakika na maisha yake ni lazima awe na uhakika wa matibabu.
Alisema kuwa kutokana na umuhimu wa mpango huo, anaagiza Viongozi wa Mkoa wa Kigoma kuhakikisha wanalibeba suala la vifurushi hivi vya bima ya afya kwa kwenda nyumba kwa nyumba ili kuelimisha na kuhimiza wananchi kujiunga.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma, Bw. Amandus Zambia alisema kuwa kitendo cha mwananchi kujiunga na vifurushi ni kuishi kwa mpango na malengo yanayomfikisha kwenye maendeleo.
“Tunaweza kabisa kujiunga endapo tutakuwa na malengo na katika hili tuwe kama watalii ambao huwekeza fedha na kuzitumia kwa kipindi fulani kutimiza lengo lao la kutalii. Hivyo nasi tuwe na malengo na tuchangamkie sana mpango wa vifurushi kwa ajili ya afya zetu na familia zetu,” alisema Bw. Zambia.