Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Mbozi, limeendelea kutoa elimu ya masuala ya usalama kupitia Kampeni ya “Tuwaambie Kabla Hawajaharibiwa” ikiwa ni jitihada za kuzuia mmomonyoko wa maadili na kuwalinda watoto na vijana dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Kampeni hiyo imeendelea leo Desemba 07, 2024 katika Chuo cha Afya Yohana Wavenza kikichopo kata ya Igamba Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe ikiwa na lengo la kuelimisha wanafunzi kuanzia ngazi ya Shule za msingi hadi Vyuo Vikuu namna ya kujiepusha na tabia hatarishi kama vile matumizi ya dawa za kulevya, ulevi na athari za kushiriki mapenzi katika umri mdogo.
Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Happy Lumbe ambaye ni Kaimu Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto akizungunza na wanafunzi wa mwaka wa kwanza chuoni hapo alisema kuwa, ukatili wa kijinsia na utandawazi umekuwa na athari kubwa kwa watoto na vijana, kwani unaleta tamaduni ambazo hazina faida kwa jamii zetu.
“Ni muhimu kuzingatia faida za utandawazi na kujua athari zake ili kuziepuka tumieni simu janja kuwapatia mahalifa kwa faida ya masomo yenu ndio maana hii leo nimekuja hapa kuwaambia kabla hamjaharibiwa na kujiingiza kwenye makundi ambayo mtakuja kujutia kutokana na tabia mbalimbali zenye kuhatarisha usalama wenu,” amesema Mkaguzi Lumbe.
Kwa upande wake Sajenti Merina Method kutoka Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Mbozi alisema kampeni ya “Tuwaambie Kabla Hawajaharibiwa” imekuja kwa lengo la kuwatahadharisha dhidi ya tabia zinazoweza kuharibu mustakabali wa maisha yenu ili muweze kutimiza ndoto za maisha yenu kwa kufanya yale yakiyo mema na kuacha matendo yote mabaya ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za uhalifu, wahalifu na ukatili wa kijinsia ili zishughulikiwe na Jeshi la Polisi.
Naye, Koplo Gladness Sizya alisema jamii inatakiwa kuwalinda wanafunzi na watoto kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kukemea vitendo vibaya dhidi yao ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za ukatili wa kijinsi ili kukinda taifa la leo na kesho dhidi ya athari zinazoendekea kushamili katika ulimwengu wa sasa hasa ulawiti, ushoga na kuiga tamaduni za nje.
Kwa upande wake, Koplo Ally Nduka kutoka Ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Songwe, alisema kuwa jamii inapaswa kutokufumbia macho vitendo vya mmomonyoko wa maadili vinavyotokana na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ili kupambana kwa ukaribu na mapambano dhidi ya mmomonyoko wa maadili ili kupata taifa lenye tija kwa maendeleo ya nchi.
Nao, walimu wa chuo hicho wamelishukuru Jeshi la Polisi na wameahidi kutimiza wajibu wao wa malezi kwa wanafunzi hao ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwapa elimu ya mambo hayo kupitia kitengo cha malezi ili wanafunzi hao watimize walichokifuata chuoni hapo.