Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
“Kwa miaka mingi tuliteseka na vibatari na chemli, tukishindwa kufikiria maisha bor, lakini kufikia 2018/2019, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitukomboa,” anasema Asiah Hussein, mkazi wa kijiji cha Mbwidu, kata ya Ubena,Jimbo la Chalinze, Mkoani Pwani.
Kwa Asiah, umeme sio tu uliangazia nyumba yake, bali pia ulifungua milango ya fursa za kiuchumi, “Nimefungua duka langu na sasa biashara yangu inakua kwa kasi, hali ni tofauti kabisa na awali,” anasema kwa furaha.
Huduma hii ya nishati imeleta Mapinduzi makubwa, si kwa maisha ya kaya bali pia kwa huduma za afya, Asiah anasimulia jinsi walivyolazimika kutumia mishumaa na vitochi kwenda zahanati usiku, “Sasa historia imebadilika kabisa, kwani watalaam wa afya wanafanya kazi kwa ufanisi, bila vikwazo vya giza,”
HALI YA UPATIKANAJI UMEME MKOANI PWANI
Mkoa wa Pwani, unaojulikana kwa viwanda vingi, unatumia megawati zaidi ya 132, ukiongozwa na Dar es Salaam inayotumia zaidi ya megawati 500, Mkoa huu una vijiji 417, ambapo asilimia 98 ya vijiji hivi tayari vimeunganishwa na umeme kupitia miradi ya awali kama vile Wakala wa Nishati Vijijini REA I ,REA II,REA III Mzunguko wa I,Peri-Urban,Ujazilizi na REA III Mzunguko wa II.
Mhandisi Jones Olotu, Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, anaeleza kuwa REA inaendelea kutekeleza miradi ya kusambaza umeme, lengo likiwa ni kuboresha maisha ya wakazi wa vijijini.
Kadhalika Vijiji 10 ambavyo havina umeme vipo kwenye maeneo ya Delta katika wilaya ya Kibiti (vijiji vitano) na visiwa katika wilaya ya Mkuranga vijiji vitatu na Mafia vijiji viwili.
Vijiji vitano kati ya kumi vilivyopo kwenye Delta ya Kibiti mkandarasi ameshasanifu,vifaa vimewasili eneo la mradi na kazi inaendelea.
Hata hivyo Olotu alieleza kuwa, Vijiji kumi Kibiti vitano, Mkuranga vitatu Mafia viwili,viko kwenye mpango wa kupatiwa umeme wa Nishati mbadala kupitia miradi ya off -grid kwakuwa ni visiwa.
Olotu anafafanua kuwa, kwa upande wa vitongoji mkoa una jumla ya vitongoji 1,135 vimekwisha kupatiwa umeme sawa na asilimia 55.6, vitongoji 135 kati ya 910 vilivyosalia vitapatiwa umeme kupitia mradi wa vitongoji vya majimbo.
Alieleza, Vitongoji 22 vitapatiwa umeme kupitia mfumo wa umeme jua kwa kuwa vipo maeneo ya visiwa, vitongoji 753 vilivyobakia vitaendelea kupatiwa umeme kupitia miradi ya umeme vitongojini kulingana na upatikanaji wa fedha.
Vilevile Olotu, alieleza kwasasa Wakala wa Nishati Vijijini unatekeleza jumla ya miradi minne yenye thamani ya bilioni 59.129.857.3 kati ya miradi hiyo ni pamoja na usambazaji wa umeme katika Vitongoji awamu ya II (HEP II).
Alibainisha, REA imeanza usambazaji wa umeme katika vitongoji awamu ya pili (HEP II) ambapo utapeleka umeme kwenye vitongoji 135 kwenye majimbo Tisa, Mkoani Pwani kwa gharama ya sh.bilioni 14.983.7.
Olotu alieleza, Mradi huu utafikia vitongoji 15 katika kila jimbo Mkoani humo na unatekelezwa na mkandarasi M/s China Railway Construction Electrification Bureau Co.Ltd .
Miradi mingine ni, mradi wa REA awamu ya tatu Mzunguko wa pili (REA II) round II na mradi wa kupeleka umeme kwenye migodi midogo na maeneo ya kilimo na mradi wa kupeleka umeme kwenye vituo vya afya na pampu za maji.
HALI YA UPATIKANAJI UMEME KWA WILAYA
Hali ya upatikanaji wa umeme katika wilaya za mkoa wa Pwani kiwilaya ikiwemo Chalinze ina vijiji 74, vyote vikiwa na umeme, na vitongoji 478 ambapo vitongoji 265 pekee vina umeme.
Wilaya ya Bagamoyo ina vijiji 8 vyenye umeme, kati ya vitongoji 174, vitongoji 116 vina umeme, wilaya ya Kibaha ina vijiji 26, vyote vikiwa na umeme, na vitongoji 100 ambapo vitongoji 83 vina umeme.
Kibiti ina vijiji 65, vijiji 60 vikiwa na umeme, na vitongoji 268, huku vitongoji 114 vikiwa na umeme ,katika wilaya ya Kisarawe ina vijiji 58, vyote vina umeme, na vitongoji 235 ambapo vitongoji 120 vina umeme na Mafia yenye vijiji 23, vijiji 21 vina umeme, na vitongoji 136 ambapo vitongoji 96 vina umeme.
Kwa upande wa wilaya ya Mkuranga, kuna vijiji 125, na kati ya hivyo, vijiji 122 vina umeme, huku Rufiji ikiwa na vijiji 38 vyote vikiwa na umeme, kati ya vitongoji 178, vitongoji 123 vina umeme.
Mkuu wa mkoa wa Pwani, Alhaj Abubakar Kunenge, aliwataka wakuu wa wilaya zote mkoani humo kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya nishati ya umeme ili kuhakikisha inafikia malengo na kuleta tija.
Aliwasisitiza wakandarasi kuhakikisha kuwa miradi hiyo inatekelezwa kwa viwango na kukamilika kwa wakati kulingana na mikataba yao.
Kunenge pia aliitaka REA kuangalia namna ya kutatua changamoto ya upatikanaji wa umeme kwenye maeneo ya visiwa ambayo bado hayajapata huduma hiyo, ili kuongeza mchango wake katika uchumi wa bluu.
Alibainisha kuwa kuna mahitaji makubwa ya umeme katika maeneo ya visiwa kwani wananchi wengi wanajihusisha na shughuli za uvuvi, na umeme utakuwa mkombozi kwao.
Mbunge wa viti maalum wa mkoa wa Pwani, Subira Mgalu, aliwahimiza wananchi kutumia nishati ya umeme ili kukuza uchumi wao.
Alieleza kuwa ,umeme ni chanzo muhimu cha maendeleo katika kila sekta, na matumizi sahihi ya nishati hii yatachochea ustawi wa wananchi.
Mbunge wa jimbo la Chalinze, Ridhiwan Kikwete, alishukuru serikali kwa kusogeza huduma ya umeme katika vijiji na vitongoji vya Chalinze, akisema kuwa eneo hilo limepata mabadiliko makubwa kwa sasa.
WAKALA WA NISHATI VIJIJINI (REA)
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inasema hali ya upatikanaji wa umeme vijijini imeongezeka kutoka asilimia 2 mwaka 2007 .
REA inatarajia kusambaza huduma ya umeme katika vitongoji 31,532 vilivyosalia nchini, ili kuboresha hali ya maisha ya wananchi wa vijijini kwa kuongeza upatikanaji wa nishati.
Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy, alieleza ili kufikisha umeme kwenye vitongoji vilivyosalia, REA inahitaji kujenga njia za umeme wa msongo wa kati zenye urefu wa kilomita 41,593 na kilomita 87,206 za msongo mdogo, kufunga mashine umba (transformers) 31,532 na kuunganisha wateja wa awali 1,552,343. Mradi huu unakadiriwa kugharimu sh. bilioni 6,701.75.
Alieleza, tangu mwaka 2008 hadi 2020, REA imekamilisha miradi mikubwa 15 ya Gridi ya Taifa na sasa inaendelea kutekeleza miradi mingine mikubwa saba iliyoanzishwa mwaka 2021.
Kukamilika kwa miradi hiyo kutahakikisha vitongoji 9,480 na wateja wa awali 534,906 wanapata huduma za umeme kupitia ujenzi wa kilomita 26,379 za njia za umeme wa msongo wa kati, kilomita 26,145 za msongo mdogo, na usimikaji wa mashine umba 9,161, kwa gharama ya shilingi trilioni 2.3.
“Lengo la kuanzishwa kwa REA mwaka 2007 lilikuwa ni kuharakisha upatikanaji wa nishati bora vijijini ili kuboresha hali ya maisha ya wananchi, kuchangia ukuaji wa uchumi, kuboresha huduma za kijamii, kuhifadhi mazingira, na kuimarisha usawa wa kijinsia na upatikanaji wa umeme,” alisema Saidy.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, Mhandisi Thomas Mmbaga, hadi sasa usambazaji wa umeme vijijini umefikia asilimia 80 tangu kuanza kwa utekelezaji wa Mradi wa Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili mwezi Julai 2018. “Ni vijiji 758 tu vilivyobaki kati ya vijiji 12,315 nchi nzima, na wakandarasi waliopewa zabuni wamekamilisha zaidi ya asilimia 75 ya kazi,” alieleza.
Katika ziara ya mkoa wa Pwani kukagua maendeleo ya mradi huo, Mhandisi Mmbaga aliongeza ,kuanzia mwaka 2024, REA itaanza kusambaza umeme kwenye vitongoji, ambapo baada ya kukamilisha vijiji vilivyosalia, vitongoji 3,060 vitapatiwa huduma ya umeme.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati ya Umeme Vijijini (REB), Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu, alionesha kuridhishwa na utekelezaji wa mradi huo. “Katika ziara yangu ya wilaya za Mkuranga, Kisarawe, Kibiti, na Rufiji, nimeona mafanikio makubwa. Huduma ya umeme imefikia zaidi ya asilimia 90 katika maeneo haya, ingawa bado kuna changamoto za kijiografia,” alisema.
WIZARA YA NISHATI
Waziri wa Nishati, ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu, Dotto Biteko, alieleza Serikali imelenga kuhakikisha vijiji vyote vinapatiwa umeme ifikapo 2025.
Kuhusu Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili (REA III Round II), Waziri Biteko alisema kuwa serikali inaendelea kutekeleza mradi huo ili kukamilisha kusambaza umeme kwenye vijiji 4,071 vilivyosalia kati ya vijiji 12,318.
Hadi Machi 2024, jumla ya vijiji 11,837 sawa na asilimia 96.37 ya vijiji vyote Tanzania Bara vilikuwa vimeunganishwa na huduma ya umeme.
Katika mpango wa kusambaza umeme katika vitongoji (Hamlet Electrification Project – HEP), serikali inaendelea na utekelezaji wa azma hiyo na inatarajia kukamilisha mradi huo ifikapo Juni 2025.
HITIMISHO
Hatua kubwa imepigwa kuboresha upatikanaji wa nishati ya umeme nchini, hususan vijijini, ambapo juhudi hizi zinachangia kwa kiasi kikubwa kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii.
Mkoa wa Pwani ni mfano bora wa jinsi miradi ya umeme inavyobadilisha maisha ya wananchi, kutoka kwenye mwanga wa vibatari kipindi cha nyuma hadi kufurahia fursa mpya za biashara, elimu, na huduma bora za afya, umeme umekuwa chachu ya maendeleo.
Hata hivyo, kuna changamoto zilizobaki, hususan maeneo ya Visiwa na Vitongoji ambavyo bado havijafikiwa kikamilifu.
Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea na jitihada za kuhakikisha vijiji na vitongoji vyote vinafikiwa na umeme ifikapo mwaka 2025, hatua ambayo itaongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii.
Mwananchi mmoja mmoja, wakiwemo wajasiriamali kama Asiah Hussein, ni miongoni mwa wanufaika wakubwa wa mapinduzi haya ya nishati, ni wazi kwamba, kwa uwekezaji na usimamizi bora, umeme utaendelea kuwa nguzo kuu ya maendeleo endelevu nchini Tanzania.