Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanal Ahmed Abbas,akisalimiana na na wachezaji wa Timu ya Bombambili United kabla ya mchezo wa fainali wa mashindano ya Ruvuma Vijana Cup yaliyoandaliwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya vijana ya Chama cha Mapinduzi(UVCCM)Mkoa wa Ruvuma Kelvin Challe kati ya Timu hiyo na Bombambili City, mchezo fainali uliyochezwa katika uwanja wa shule ya msingi Sokoine Manispaa ya Songea ambapo Bombambili United iliibuka mabingwa baada ya kuifunga Bombambili City kwa Penati 4-2
Na Muhidin Amri,
Songea
MKUU wa mkoa wa Ruvua Ahmed Abbas,amewataka wakazi wa mkoa huo hususani vijana kutumia mabonanza mbalimbali ya michezo kuhamasishana na kuelimishana juu ya umuhimu wa kwenda kujiandikisha kwenye Daftari la orodha la wapiga kura.
Alisema,kujiandikisha kwenye Daftari hilo kutawawezesha kuwa na sifa ya kupiga kura na kuchagua viongozi bora wanaowataka kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajia kufanyika tarehe 27 Novemba mwaka huu.
Kanali Abbas amesema hayo jana,wakati akifunga fainali ya mashindano ya Ruvuma vijana (vijana Ruvuma Cup 2024) kati ya Timu ya Bombambili City na Bombambili United iliyochezwa katika uwanja wa shule ya msingi Sokoine Manispaa ya Songea.
Aidha alisema,vijana wa mkoa wa Ruvuma wanapaswa kutumia mchezo huo kama hamasa ya kuendeleza michezo mingine hasa ikizingatiwa kuwa hivi sasa michezo imesaidia watu wengi kupata ajira.
Amempongeza mwenyekiti wa umoja wa vijana wa Chama cha Mapinduzi Kelvin Challe, kwa ubunifu wake mkubwa wa kuanzisha mashindano hayo yaliyowakutanisha vijana wengi kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Ruvuma.
Abbas,amewashukuru wadau waliosaidia kufanikisha mashindano ya vijana akiwemo Mbunge wa Vijana na Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga aliyetoa jezi kwa timu zote zilizoshiriki Ligi hiyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Ruvuma Kelvin Challe,amewashukuru wananchi waliopata nafasi ya kushiriki Ligi hiyo kuanzia hatua ya awali hadi fainali.
Alisema,jambo la kujivunia mashindano ya mwaka huu yamekuwa yenye hamasa na mwitikio mkubwa kwani imeshirikisha jumla ya timu 32 ikilinganisha na msimu uliopita hasa baada ya kuongezeka kwa zawadi kwa washindi na timu zote shiriki.
Alisema, mwaka huu mshindi wa kwanza amepata Sh.milioni 3 mshindi wa pili milioni 2, timu iliyoshika nafasi ya tatu imepata Sh.milioni 1 na timu zote zimepata zawadi ya jezi seti moja.
Amewaomba vijana ambao bado hawajajiandikisha katika Daftari la wapiga kura,kutumia siku chache zilizobaki kuhakikisha wanakwenda kwenye vituo vilivyotengwa kwa ajili ya kujiandikisha ili wapate nafasi ya kuchagua viongozi kwenye vijiji na mitaa wanakoishi.
Awali Mkuu wa wilaya ya Songea Kapenjama Ndile,amempongeza Mwenyekiti huyo kwa kuwaunganisha vijana wengi wa mkoa wa Ruvuma kupitia sekta ya michezo.
Katika mchezo wa fainali uliochezwa katika uwanja wa Shule ya msingi Sokoine,Timu ya Bombambili United imeibuka bingwa baada ya kuifunga Timu ya Bombambili City kwa Penati 4-1 baada ya kutoka sale bila kufungana ndani ya Dakika 90 .