Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwanza kufunga Mkutano Mkuu wa Kumi wa Wadau wa Lishe kwenye ukumbi wa Malaika Beach Resort jijini Mwanza, Oktoba 3, 2024. Wa pili kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi na kulia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Michael Lushinge Masanja. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama mtambo wa kuchanganya lishe katika vyakula alipotembelea banda la maonesho la Taasisi ya GAIN Tanzania kabla ya kufunga Mkutano Mkuu wa kumiwa Wadau wa Lishe kwenye ukumbi wa Malaika Beach Resort jijini Mwanza, Oktoba 3, 2024. Wa pili kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi na kushoto ni Meneja Mradi wa GAIN Tanzania, Archard Ngemera. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama mtambo wa kuchanganya lishe katika vyakula alipotembelea banda la maonesho la Taasisi ya GAIN Tanzania kabla ya kufunga Mkutano Mkuu wa Kumi wa Wadau wa Lishe kwenye ukumbi wa Malaika Beach Resort jijini Mwanza, Oktoba 3, 2024. Wa tatu kushoto ni Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel na kushoto ni Meneja Mradi wa GAIN Tanzania, Archard Ngemera. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Afisa Lishe, Amasidze Buhela alipotembelea banda la maonesho la Taasisi ya COUNSENUTH Tanzania kabla ya kufunga Mkutano Mkuu wa Kumi wa Wadau wa Lishe kwenye ukumbi wa Malaika Beach Resort jijini Mwanza, Oktoba 3, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Afisa Lishe wa Jiji la Mbeya, Itika Mulagalila (wa tatu kushoto) katika maonesho ya lishe mbalimbali kabla ya kufunga Mkutano Mkuu wa Kumi wa Wadau wa Lishe kwenye ukumbi wa Malaika Beach Resort jijini Mwanza, Oktoba 3, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza alipofungua Mkutano Mkuu wa Kumi wa Wadau wa Lishe kwenye ukumbi wa Malaika Beach Resort jijini Mwanza, Oktoba 3, 2024.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi ya Washiriki wa Mkutano Mkuu wa Kumi wa Wadau wa Liste wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipofunga mkutano huo kwenye ukumbi wa Malaika Beach Resort jijini Mwanza, Oktoba 3, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuwa suala ya lishe ni kipaumbele muhimu kwa Serikali katika kuwezesha utekelezaji wa mipango ya maendeleo na shughuli za kiuchumi kwa jamii jamii zikiwemo za kilimo, uvuvi, ufugaji na biashara.
Amesema hayo leo (Alhamisi, Oktoba 03, 2024) wakati alipofunga Mkutano Mkuu wa Kumi wa Wadau wa Lishe kwenye ukumbi wa Malaika Beach Resort jijini Mwanza.
Amesema kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kutokomeza aina zote za utapiamlo nchini. “Mheshimiwa Rais Dkt. Samia amedhihirisha dhamira yake ya dhati ya kulipa umuhimu wa kipekee suala la lishe.
Hatua ambayo imemfanya awe kinara na mmoja wa viongozi wanaotambuliwa na kutolewa mfano ulimwenguni kwa hatua ambazo wameweza kupiga katika mapambano dhidi ya changamoto za utapiamlo”
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wadau wote wa lishe wahakikishe wanatumia vizuri matokea ya ripoti ya mapitio ya muda wa kati ili kujitathmini na kuchukua hatua stahiki za kuboresha utekelezaji wa afua za lishe.
Pia, Waziri Mkuu ameziagiza mikoa na halmashauri zote nchini itumie mwongozo wa Kitaifa wa utoaji wa huduma ya chakula na lishe kwa wanafunzi wa elimu ya msingi na wahakikishe matumizi ya vyakula vilivyorutubishwa yanajumuishwa na kutengewa fedha katika mipango na bajeti za kila mwaka.
“Ofisi ya Rais – TAMISEMI hakikisheni kuwa mikataba ya lishe kati ya Mheshimiwa Rais na Wakuu wa Mikoa inatekelezwa kikamilifu na kuwa na tija. Endeleeni kufanya ufuatiliaji wa karibu na kutoa taarifa za utekelezaji mara kwa mara.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amezitaka wizara, wakala, taasisi na mashirika ya umma watumie kikamilifu mwongozo wa mpango jumuishi wa Taifa wa lishe na bajeti na kuhakikisha masuala ya lishe yanajumuishwa katika mipango na kutengewa fedha ili yatekelezwe kikamilifu kila mwaka.
Kwa Upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi amesema kuwa mkutano huo umekutanisha wadau wa lishe wanaotekeleza masuala ya lishe kutoka sekta za umma, binafsi na washirika wa maendeleo.
Waziri Lukuvi amesema lengo la mkutano huo ni kujadili kwa kina mafanikio na changamoto zilizopo katika utekelezaji wa afua za lishe nchini na kutathimini hatua iliyofikiwa kulingana na malengo yaliyowekwa kwenye mpango jumuishi ya pili ya lishe.
“Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kuratibu utekelezaji wa mpango huo jumuishi ulioanza mwaka 2021/22 na sasa tumeona mafanikio makubwa ambayo kama wadau walishe tumeyapata katika mwaka wa pili wa utekelezaji wake”
Naye, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema masuala ya lishe yana mchango mkubwa katika afya za watu hivyo ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuendelea kuratibu masuala hayo.“Lishe ni muhimu, tunatakiwa tulichukue suala hili kwa umuhimu mkubwa, tukizingatia masuala ya lishe tutapunguza wagonjwa mawodini.”
Awali, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amesema kuwa wanaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali kupitia Shirika la Kuendeleza Viwanda Vidogo (SIDO) na kuhakikisha wanaleta teknolojia rahisi ya kuongeza virutubisho kwenye vyakula ili jamii ya Watanzania hususani watoto wapate lishe bora.
“Sisi kama Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na wadau wengine tunahakikisha tunaendelea kurahisisha teknolojia ambazo zitaleta afua ili kila mmoja apate lishe bora kupitia teknolojia rahisi ambazo tunaamini wengi wetu wanaweza kutumia.”