AFISA Mtendaji Mkuu wa WazoHuru Media Ndg Mathias Canal amechangia jumla ya Shilingi Milioni 5 kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili shule ya Msingi Tutu iliyopo katika Kata ya New Kiomboi, Wilayani Iramba katika mkoa wa Singida.
Akizungumza wakati wa Mahafali ya 70 ya shule hiyo iliyofanyika tarehe 1 Octoba 2024, Mathias Canal ametaja maeneo aliyochangia kuwa ni pamoja na madawati 37 yenye thamani ya Shilingi Milioni 3.15, vifaa vya michezo vya Shilingi 800,000 (Jezi jozi mbili pamoja na mipira 4), pamoja na shilingi Milioni 1 kwa ajili ya kuunganisha na huduma ya umeme shule hiyo.
Mathias amesema kuwa Kukosekana kwa huduma ya umeme katika shule hiyo kunasababisha wanafunzi kushindwa kujifunza baadhi ya mada kwa vitendo (uhalisia) jambo linalorudisha nyuma juhudi za walimu na wanafunzi kwa ujumla wake katika kujiimarisha kielimu.
Kuhusu changamoto ya madawati na vifaa vya michezo amesema kuwa ili mwanafunzi awezi kufaulu anahitaji utulivu wa mwili na akili hivyo kukaa chini kunamfanya kuchukia masomo na shule badala yake wakikaa kwenye madawati kunaongeza hamasa ya kuipenda elimu. Hata hivyo amesema kuwa miongoni mwa mambo muhimu kwa wanafunzi ni pamoja na kuimariaha sekta ya michezo.
“Kama inavyofahamika kwamba michezo ni afya na ajira. Hivyo ukosefu wa vifaa vya michezo kama mpira wa miguu, mpira wa pete, mpira wa wavu, mpira wa mikono pamoja na jezi na vifaa vyingine mbalimbali vya mchezo kunarudisha nyuma juhudi za kuimarisha sekta ya elimu kupitia michezo” Amesisitiza Canal
Katika mahafali hayo Mathias ameungwa mkono na Mkurugenzi mweza wa kampuni ya WazoHuru Media Ndg Riziki Charles Nkwiga pamoja na Mkurugenzi wa DM Planet Ndg David Mtengile kwa kuchangia jumla ya Shilingi 600,000 kwa ajili ya madawati sambamba na kuchangia kiasi cha Shilingi 348,500 kwa ajili ya kuwapeleka wanafunzi pamoja na walimu mjini Singida kujifunza kwa vitendo na kujionea vivutio vya utalii ikiwemo ziwa Singidani, Ziwa Kindai na Ziwa Monabang’i.
Aidha, amewapongeza wananchi kwa kujitolea kuchangia ujenzi wa madarasa mawili na ofisi ya walimu na kuwasihi kuendelea kuiunga mkono serikali katika jitihada mbalimbali za kuboresha elimu ikiwemo ujenzi pamoja na michango kwa ajili ya wanafunzi ili waweze kupata chakula shuleni.