********************************
28 Desemba, 2019
Katibu Mkuu wa Chama Chama Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally amezitaka Kamati za Siasa za Wilaya na Mikoa kuwasilisha maoni yao ya namna ya kuboresha maisha ya wananchi kabla ya tarehe 15 Januari, 2020 yaweze kujumuishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025.
Katibu Mkuu ameeleza kuwa, moja ya maelekezo ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ni kuzitaka Kamati za siasa za wilaya na mikoa kuwasilisha maoni ya wananachi wote katika kuboresha maisha yao, ili yaingie kwenye miaka kumi ya Mwelekeo wa Sera za CCM 2020 – 2030 na Ilani ya CCM ya mwaka 2020 – 2025 na mwisho wa kuwasilisha maoni hayo ni tarehe 15 Januari, 2020.
Katibu Mkuu ameyasema hayo leo tarehe 28 Desemba, 2019 akiwa katika kikao cha Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Kagera kikijumuisha wajumbe wa Kamati za siasa na sekretariet za Wilaya ya Bukoba Mjini, Vijijini na Misenyi.
“Moja ya maelekezo ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa iliyokaa mwezi Desemba mwaka huu, ni kuziagiza Kamati za Siasa za Wilaya na Mikoa kukusanya maoni ya wananchi katika maeneo yao ya namna ya kuboresha maisha ya watu katika sekta mbalimbali ili yaingie kwenye Mwelekeo wa miaka kumi wa Sera za CCM na Ilani ya CCM 2020 – 2025 na mimi ndio msimamizi wa maelekezo hayo.” Dkt. Bashiru amesisitiza
Ameongeza kuwa, katika kipindi hiki cha kukusanya maoni ya wananchi ili Ilani iwe jumuishi, wananchi wote wanaruhusiwa kutoa maoni iwe walimu, madaktari, wafanyabiashara, wakulima na hata wale wa vyama vya Upinzani, kwani CCM kwa namna inavyoendelea kutekeleza matakwa ya wananchi, mwaka 2020 itashinda, hivyo ni vema mawazo ya wanachama wa vyama hivyo nayo yakajumuishwa mapema kwa utekelezaji.
Wakati huo huo Katibu Mkuu ameendelea kusisitiza umuhimu wa umoja na mshikamo miongoni mwa wanachama na viongozi wote ili kuendelea kulinda heshima na nidhamu ya CCM.
Aidha Dkt. Bashiru amewatembelea wasisi wa Chama Wilayani Bukoba ikiwa ni utamaduni wa CCM kuwajulia hali wazee, kujua changamoto zao, na kuenzi mchango wao katika ujenzi wa Chama na Taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu akiwa na Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Ndg. Ngemela Lubinga ambaye naye yupo mapumzikoni wilayani Misenye, ametembelea ujenzi wa Ofisi ya CCM kata ya Bwanjai Wilaya Misenyi na kuchangia shilingi milioni mbili ikiwa ni kuunga mkono juhudi za wanachama katika kuimarisha Chama
Ziara hiyo imejumuisha viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kagera mama Constancia Buhiye
Katibu Mkuu ameendelea na mapumziko ya siku kumi nyumbani kwake, Bukoba Mkoani Kagera na anatarajiwa kumaliza mapumziko hayo mwanzoni mwa mwezi Januari, 2020.