Na; Mwandishi Wetu – Mwanza
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete amehimiza vijana kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa unatarajiwa kufanyika Novemba 2024.
Mhe. Ridhiwani ameyasema hayo leo Septemba 26, 2024 jijini Mwanza wakati akizungumza na makundi mbalimbali ya vijana ikiwamo wasanii, wanamuziki, waigizaji, wamachinga na waandishi wa vitabu katika ziara yake mkoani humo ya kukagua maandalizi ya kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru 2024.
“Vijana wenzangu jitokezeni mkagombee nafasi hizi sio za watu fulani sisi ndo tunaojua mahitaji yetu kama vijana, hivyo hakikisheni mnajiandikisha kwenye daftari la wapigakura ili kuweza kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa tukachague viongozi bora,” amesema.
Vilevile, Mhe. Ridhwani amehamasisha vijana hao kushiriki katika maadhimisho ya wiki la vijana kitaifa yatakayofanyika jijini Mwanza kuanzia Oktoba 8 hadi 14, 2024 ili kujionea shughuli zinazofanywa na vijana wenzao, taasisi na wadau wanaoshughulikia masuala ya maendeleo ya vijana. Sambamba na hayo amesema kuwa wiki hiyo itaambatana na kongamano la vijana ambalo litashirikisha vijana kutoka Tanzania Bara na visiwani.
Katika ziara hiyo, Mhe. Ridhiwani Kikwete amekagua maendeleo ya vijana wa halaiki katika uwanja wa CCM Kirumba yatakapofanyika maadhimisho ya kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2024; uwanja wa Furahisha itakapofanyika wiki ya vijana na Kanisa la Nyakahoja Parokia ya Mtakatifu Fransisco Xavier (Jimbo kuu la Mwanza) itakapofanyika ibada ya maalumu ya kumuombea Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
Waziri Kikwete aliambatana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Mhe. Tabia Mwita, Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana ya masuala ya vijana Zanzibar, Fatma Rajab, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Eliakim Mtawa na Mkurugenzi wa Vijana Zanzibar, Shaib Mohamed.