Viongozi wa serikali za mitaa wilaya ya Ilemela wametakiwa kuyatambua na kuyalinda maeneo ya wazi kwaajili ya shughuli za kijamii badala ya kuyaacha yakavamiwa na kuporwa na watu wasiokuwa waaminifu
Rai hiyo imetolewa na mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula wakati wa ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya jimbo hilo aliyoifanya katika kata za Pasiansi na Kawekamo ambapo amewataka wenyeviti na watendaji wa mitaa kuchukua hatua za haraka wanapoona maeneo ya wazi yanavamiwa na kujengwa
‘.. Hatuwezi kuacha watu wafanye wanavyotaka alafu mwisho wa siku tunaanza kulalamika maeneo ya wazi yanavamiwa wakati wanaanza kuingia sie tupo na tunawaangalia ..’ Alisema
Aidha Mhe Dkt Mabula amemshukuru na kumpongeza Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya jimbo lake ambapo mpaka sasa manispaa ya Ilemela imekwisha pokea zaidi ya bilioni 65 kwaajili ya utekelezaji wa miradi balimbali ya maendeleo
Diwani wa kata ya Pasiansi Mhe Rosemary Mayunga na diwani wa kata ya Kawekamo Mhe Omary Bakari kwa nyakati tofauti wamemshukuru mbunge wa jimbo la Ilemela kwa ziara zake kwani zimekuwa chachu katika kuongeza kasi ya ukamilishaji wa miradi ya maendeleo katika kata zao huku wakiwataka wananchi wa kata zao kuchangia na kushirikiana na serikali kuanzisha miradi mipya
Kwa upande wake afisa ardhi manispaa ya Ilemela Ndugu Ismail Kalaghe amefafanua kuwa ni jukumu la wananchi wote kulinda maeneo ya umma huku akiwaahidi kuendelea kutatua kero za ardhi zilizolalamikiwa na wananchi hao hasa kuhusu ulipwaji wa fidia kwa maeneo yaliyotwaliwa na serikali kwa shughuli za umma ambapo mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Bi Ummy Mohamed Wayayu amekuwa na utaratibu wa kutenga fedha za mapato ya ndani na kulipa madeni ya fidia
Joachim George ni mwananchi wa kata ya Kawekamo ambapo licha ya kuipongeza serikali kwa kazi kubwa ya maendeleo, ameomba kupewa kipaumbele zoezi la ulipaji wa fidia kwa wananchi kwani wengine wamefariki kabla hata ya malipo ya fidia zao huku wengine wakiugua kutokana na msongo wa mawazo unaotokana na kucheleweshwa kwa fedha za malipo ya fidia hizo
Mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula ataendelea na ziara yake leo septemba 19 katika kata za Ilemela na Buzuruga kusikiliza kero za wananchi na kukagua miradi ya maendeleo