Na. Zillipa Joseph, Katavi
Wanafunzi 296 wa shule ya msingi Inyagantambo katika kata ya Tongwe halmashauri ya wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi wamepata madarasa ya kudumu baada ya kusoma katika madarasa ya nyasi na wanafunzi wengine wakisomea chini ya miti kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitatu.
Kuanzishwa kwa shule ya msingi Inyagantambo lilikuwa wazo la wakazi wa kitongoji hicho baada ya kuona watoto wao wanatembea umbali wa zaidi ya kilomita 16 kwa siku kufuata shule ya msingi Mpanda Ndogo.
Hali ya kutembea umbali mrefu ilikuwa ikikatisha tamaa wanafunzi walio wengi na wengine walishindwa kumaliza elimu ya msingi.
Shule ya msingi Inyagantambo (ambayo ilikuwa ni shule shikizi) ilikuwa na wanafunzi 136 wa darasa la awali hadi darasa la tatu na walimu wanne wa kujitolea.
Full Shangwe ilifika shuleni hapo mapema mwaka uliopita na kusikiliza kilio cha walimu hao wa kujitolea na wanafunzi ambao waliiomba serikali kuwajengea shule.
Kilio chao kilifika kwa mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu ambaye aliamua kufanya ziara kujionea hali halisi ya shule hiyo akiwa ameambatana na wataalam mbalimbali wa ofisi yake.
Baada ya siku chache mkuu huyo wa wilaya ya Tanganyika alihamasisha wanakijiji katika zoezi la kuchimba msingi wa vyumba vya madarasa na hapo safari ya ujenzi wa madarasa nane na ofisi moja ya walimu ilianza.
Serikali ilipeleka fedha kiasi cha shilingi milioni mia nne mwezi Septemba mwaka jana kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hiyo.
Afisa Elimu Msingi wa wilaya ya Tanganyika bwana Gidion Bunto amesema shule hiyo yenye walimu nane katinyao walimu wanne wanajitolea sasa imesajiliwa na ina jumla ya wanafunzi 296 wa darasa la kwanza hadi darasa la sita.
“Tulihamisha wanafunzi wengine wa shule ya msingi Mpanda Ndogo hasa wale ambao jiografia ya makazi yao ni karibu na hapo shule mpya” alisema Bunto.
Mwaka huu ulipoanza wanafunzi walianza kuyatumia rasmi madarasa yao mapya.
“Shule hii pia itasaidia sana kuongezeka kwa wanafunzi wapya wa darasa la awali na darasa la kwanza kwa sababu shule ipo karibu na makazi ya watu” aliongeza.
Wakazi wa kitongoji hicho wanaishukuru serikali kwa kuwajengea shule.
“Madarasa ni ya kisasa tena yana vioo na marumaru” alisema Shija Butogwa mmoja wa wakazi wa Inyagantambo.
Buholo Masaga ni mama mwenye wanafunzi wawili wa darasa la kwanza na la pili alieleza kuwa kipindi cha masika alikuwa akiwahurumia watoto wake kwani madarasa yao yalikuwa chini ya mti.
Kwa upande wao walimu wa kujitolea wameiomba serikali kuwapa ajira.
“Tumefundisha chini ya mti kwa muda mrefu, tunaonba watuangalie na sisi katika ajira” alisema Mwalimu Nickson Kibende.
Nao wanafunzi wa shule hiyo wameonyesha furaha kusoma katika shule nzuri.
“Nina furaha, hata vyoo vyetu ni vizuri pia” alisema Bahati Malendeja mwanafunzi wa darasa la pili.
Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu amesema serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya elimu.
“Elimu ni msingi wa maendeleo ya kila mwanadamu, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais mama Samia Suluhu Hassan kutuletea fedha kiasi cha shilingi milioni mia nne kwa ajili ya ujenzi wa shule hii” alisema Buswelu
Mkuu wa mkoa wa Katavi Bi Mwanamvua Mrindoko amesema serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Nitoe wito kwa wazazi kuona umuhimu wa kumpeleka mtoto shule hasa mtoto wa kike. Najua huku ni kwa watani zangu wanapenda kuozesha mapema lakini atakayebainika kaoa mwanafunzi mkono wa sheria utamfikia” alisema Mrindoko.
Akizungumzia hali ya uboreshaji wa madarasa Mratibu wa mradi wa Mtoto Kwanza kutoka asasi isiyo ya kiserikali ya Lake Rukwa Development Organization (LARDEO) Philbert Chundu amesema ni jambo jema serikali kuwajali wananchi wake.
Ameendelea kuongeza kuwa serikali inaboresha sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na ongezeko la vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na miundombinu ya barabara.
Sura ya kwanza ya sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 toleo la mwaka 2023, sera hiyo imetamka kwamba serikali ina jukumu la kuandaa na kuzalisha rasilimali watu kwa ajili ya Taifa.
Sera hiyo imeendelea kufafanua kuwa suala la miundombinu, uboreshaji wa mazingira ya kufundishia na ujifunzaji yataendelea kuboreshwa ili kupata uwiano unaostahili kwa manufaa ya kujenga taifa bora la baadae.
Mratibu wa Mradi wa Mtoto Kwanza unaotekelezwa
Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kwa sasa ni ajenda ya ulimwengu ambapo huduma za MMMAM zinatambulika kuwa muhimu katika kufikia Malengo ya Maendeleo.
Huduma hizo ni pamoja na kutaka mtoto mwenye umri wa kuanzia miaka 0-8 kupata fursa ya ujifunzaji.
Hali hiyo sasa inapelekea watoto wanaopaswa kujiunga na shule hususan darasa la awali na la kwanza kupata nafasi ya kupata elimu kutokana na ongezeko la vyumba vya madarasa.