Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kupitia vituo vya utafiti vya Ukiriguru (Mwanza), Tengeru (Arusha) na Mlingano (Tanga) kwa kushirikiana na watafiti kutoka Kituo cha Kimataifa cha Utafiti wa Fiziolojia na Ikolojia ya Wadudu (icipe) kilichopo Nairobi nchini Kenya, imetoa mafunzo kwa maafisa ugani na wakulima viongozi 165 kutoka kata 31 juu ya njia husishi za kudhibiti wadudu waharibifu wa matunda ya parachichi, machungwa na embe.
Mafunzo hayo yamefanyika kuanzia Septemba 9-13, 2024 katika Wilaya za Hai, na Siha Mkoa Kilimanjaro na Muheza, Mkoa wa Tanga ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa njia husishi za kudhibiti wadudu wa miti ya matunda kwenye ikolojia mbalimbali (Fruit tree agro ecological-based IPM) ambapo katika wilaya za Hai na Siha yalijikita katika matunda ya parachichi, huku kwa Wilaya ya Muheza mafunzo yalijikita kwenye matunda ya machungwa na embe.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Dkt, Abdullah Mkiga Mtafiti kiongozi wa Mradi huo kutoka TARI Ukiriguru amesema lengo la mafunzo ni kuhakikisha wakulima wanapata elimu bora ya kudhibiti wadudu waharibifu wa matunda kama nzi na nondo wanaoshambulia matunda ambao husababisha matunda kuoza na kushusha kiwango cha mavuno na ubora.
Naye mtafiti kutoka ICIPE Dkt Shepard Ndlela amesema kupitia njia husishi za kudhibiti visumbufu mkulima ataweza kupunguza gharama na matumizi ya viuadudu vya kemikali na kuongeza mavuno na ubora kwa soko ndani na kimataifa.
Mradi wa ‘Fruit tree agro ecological-based IPM’ unatekelezwa kwa miaka mitatu (2023-2026) kupitia kituo cha TARI Ukiriguru kwa kushirikiana na taasisi ya ICIPE chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ).
Charles Semagongo mkulima wa machungwa Kijiji cha Mkinga, Wilaya ya Muheza anasema kupitia mafunzo hayo ameweza kuwatambua wadudu ambao awali alikuwa hafahamu kama ni hatarishi kwenye matunda.
Naye Fatuma Muhammed-Mkulima wa machungwa Kijiji cha Mkinga Wilaya ya Muheza, anasema mafunzo hayo yamewasaidia sio tu kutambua wadudu waharibifu bali pia kutambua wadudu rafiki kwenye uzalishjai wa matunda ambao awali walidhani ni hatarishi lakini Wataalamu wamewaeleza ni wadudu rafiki wanaozuia wadudu waharibifu kushambulia matunda na wanachangia kuongeza tija.
“Sisi tulijua hawa wadudu (jamii ya siafu) tunawaita huku kwetu “madadada” kuwa ni waharibifu wa machungwa lakini wataalamu wametueleza ni wadudu rafiki wanaozuia wadudu wengine kushambulia machungwa” alisema Fatuma.
Awali wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Wilayani Hai, Mkuu wa Wilaya hiyo Ndg Lazaro Twange aliipongeza TARI kwa kuweka nguvu katika kuwajengea uwezo wataalam wa wa kilimo na wakulima viongozi katika maeneo mbalimbali ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kuinua sekta hiyo muhimu.
Kwa upande mwingine Mkurugenzi mtendaji wa Wilaya ya Muheza Dkt Juma Mhina alisema mradi huo umekuja wakati sahihi na kwa watu sahihi akitolea mfano wa Muheza kuwa Uchumi wa wananchi wa Wilaya hiyo hutegemea machungwa na wamekuwa na kilio cha wadudu waharibifu wa matunda hayo. Kutokana na mafunzo hayo Dkt. Mhina anasema mradi utakuwa ni suluhisho la changamoto ya wadudu waharibifu huku ikichangia kipato cha wakazi wa Muheza, kuongezeka mapato ya Halmashauri na hatimaye taifa kwa ujumla kupitia Kilimo cha matunda yanayouzwa ndani na nje ya nchi.