NA MWAMVUA MWINYI,KIBAHA
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani, Humoud Jumaa, ametoa rai kwa Jumuiya ya Wanawake (UWT) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo ,kuanzisha miradi ili kujiimarisha kiuchumi na kuondokana na utegemezi.
Aidha amewaasa waendelee kuwa na umoja kwenye jumuiya pamoja na kushirikiana kuhakikisha chama kinashinda katika uchaguzi mkuu ujao wa madiwani, wabunge na Rais.
Akizungumza wakati anafungua baraza la mwaka la Jumuiya hiyo , mbele ya wabunge wa Viti Maalumu Zaynabu Vulu na Hawa Mchafu, Jumaa alieleza, hatua hiyo itasaidia kujiendeleza kimaendeleo wenyewe na kutatua mahitaji yao madogo madogo badala ya kutegemea misaada.
“Nimefarijika kuwa mgeni rasmi katika Baraza lenu la mwaka, niwapongeze kwa kazi mliyoifanya wakati wa uchaguzi wa Wenyeviti wa Serikali za Vijijini na Vitongoji, niwaombe m’buni miradi”,
“Nina marafiki wakubwa nitawaona pale penye mahitaji yatakayofaa kwenda kuwaomba kunisaidia kwa ajili ya kuendeleza biashara zenu zitazokuwa kitega uchumi kwa Jumuiya, huku nikishirikiana na wabunge wa Viti Maalumu watawaunga mkono” alisema Jumaa.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalumu Zaynabu Vullu ameendelea na ugawaji wake wa vitendea kazi kwa Jumuiya mkoani hapa, ambapo alikabidhi boksi tatu za karatasi kwa ajili ya shughuli za Jumuiya zilizoko ndani ya Chama Cha Mapinduzi kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao.
Mwenyekiti wa UWT wilayani humo, Leyla Humoud aliwashukuru wabunge wa Viti Maalumu Zaynabu Vulu, Subira Mgalu na Hawa Mchafu, kwa namna wanavyoshirikiana nao katika nyanja mbalimbali ili kuinua Jumuiya.
Leyla alitaka washikamane na kuwa wamoja kwani ndio nguzo pekee ya kusonga mbele.