NA FAUZIA MUSSA
BARAZA la Tiba asili na tiba mbadala Zanzibar, kwa kushirikiana na Wakala wa chakula na Dawa (ZFDA), wamelifungia duka la dawa asili maeneo ya kwa Hajitumbo kutokana na kuwepo kwa dawa za hospitali katika duka hilo.
Hayo yamebainika kufuatia ukaguzi uliofanywa na baraza hilo katika baadhi ya maduka yaliopo mkoa wa Mjini Magharibi.
Mrajisi wa baraza la Tiba asili na tiba mbadala Zanzibar,Mohammed Mshenga Matano akizungumza na waandishi wa habari baada ya ukaguzi huo alisema kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Aidha alieleza kuwa baraza haliridhishwi na tabia ya wafanyabiashara kama hao wanaochanganya dawa za asili na dawa za hospitali kwani mbali ya kwenda kinyume na sheria lakini pia wanahatarisha afya za jamii.
“Katika duka hili tumebaini uwepo wa dawa zisizostahiki kuuzwa hapa, kwani muuzaji hawezi kutoa maelezo sahihi ya kutumia dawa hizi zinazoelekeza zitumiwe kwa mujibu wa maelekezo ya daktari” Alisema
Alisema uzowefu unaonesha kuwa wafanyabiashara wengi wa dawa za asili hawana utaalamu wa dawa za hospitali, hivyo endapo dawa hizo zitatolewa bila muongozo wa daktari zitaleta athari kwa mtumiaji.
Mbali na hayo alieleza kuwa baadhi ya dawa hizo zimemaliza muda wa matumizi na kutoa wito kwa jamii kutumia dawa kwa ushauri na maelekezo ya daktari ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.
Alizitaja baadhi ya dawa zilizobainika katika duka hilo kuwa ni pamoja na dawa za kuongeza nguvu za kiume, pamoja na za kutibu magonjwa ya wanawake ambazo zote zinahitaji muongozo wa daktari wakati wa kuzitumia.
Alisema licha ya Baraza hilo kuchukua juhudi ya kuwapatia elimu watoa huduma za tiba mbadala wakati wa ukaguzi lakini bado baadhi ya wadau hao wanaendesha biashara hiyo kinyume na taratibu zilizowekwa.
Alieleza Kwa mujibu wa sheria namba nane ya mwaka 2008 ya baraza hilo hatua zinazopaswa kuchukuliwa kwa makosa kama hayo ni pamoja na kuziondoa sokoni dawa hizo,au kutozwa faini isiyopungua laki moja na isiyozidi laki mbili, au kifungo kisichopungua mwezi mmoja na kisichozidi miezi 6, au adhabu ya kusitisha huduma hadi taratibu zitakapokamilika au vyote kwa pamoja.
Mkuu wa divisheni ya vipodozi walala wa dawa na chakula (ZFDA), Mfamasia Salim Hamad Kassim alisema wataendelea kushirikianana na baraza la tiba asili na tiba mbadala ili kuondoa changamoto hizo na kuleta matokeo chanya kwa jamii.
Alifahamisha kuwa endapo dawa za hospitali zitahifadhiwa vibaya au kuingizwa nchini bila utaratibu unaokubalika kutaleta athari moja kwa moja kwa mtumiaji wa miwsho, hivyo ZFDA itashirikiana na kila mdau katika kulinda afya za wananchi.
Hata hivyo alilishukuru baraza hilo kwa ukaguzi wao uliosaidia kuibua maovu ya wadau wa tiba asili dhidi ya jamii, na kuishauri jamii kuacha kununua na kutumia dawa kiholela ili kulinda afya zao .
Mmiliki wa duka hilo Mwatima Bakari Mussa alikiri kufanya kosa hilo na kuiomba radhi Serikali na jamii kwa ujumla kutokana na makosa hayo aliyodai kufanywa bila kujua.
Alifahamisha kuwa duka hilo limekua likipokea dawa kutoka sehemu mbalimbali bila kuangalia uhalali na ubora wake, hivyo aliiahidi kuwa makini wakati wa kupokea dawa hizo ili kuepusha kutokea tena kwa makosa kama hayo dukani hapo.
Baadhi ya wafanyabiashara waliokua karibu na duka hilo waliwashauri wafanyabiashara wa tiba asili kujali afya za watumiaji na sio kuzingatia maslahi binafsi.
walisema uzowefu unaonesha kuwa jamii haina uelewa juu ya dawa hizo hivyo ipo haja kwa ZFDA na baraza la tiba asili kutoa elimu ili kuwasaidia kulinda afya zao.