Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza wamemchagua Diwani wa Nyamagana (CCM),Bhiku Kotecha kuwa Naibu Meya wa jiji hilo kwa kipindi kingine cha mwaka mmoja.
Uchaguzi huo umefanyika leo baada diwani huyo kumaliza muda wake,alipendekezwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya mchakato ndani ya Chama kukamilika ili kuwania nafasi hiyo aliyokuwa akitumikia.
Katika uchaguzi huo madiwani wamemchagua Kotecha kwa kura 21 kati ya 22 zilizopigwa huku kura moja ikiharibika ambapo Ofisa Uchaguzi Jiji la Mwanza, Lilian alimtangaza kuwa Naibu Meya kwa kipindi kingine cha mwak mmoja.
Uchaguzi huo umefanyika kwa mujibu wa kanuni za kudumu za Hlamashauri ya Jiji la Mwanza za mwaka 2013 kanuni namba 7 (3) ,moja ya agenda ya Mkutano Mkuu wa Mwaka ni kumchagua Naibu Meya kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2024/25.
Akizungumza baada ya kutangazwa Kotecha amewashukuru madiwani kwa kuonesha imani kubwa na kumchagua kwa kura nyingi za kishindo kuendelea kushika wadhifa huo huku akiahidi ushirikiano kwa ustawi halmashauri na wananchi wa jiji hilo.
“Kwa heshima kubwa nikishukuru Chama changu (CCM), kunipendekeza kuwania nafasi hii pia,niwashukuru madiwani kwa kuniamini na kunichagua tena.Niwaahidi ushirikiano ili tumsaidie Mh.Rais Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kazi ya kuwatumikia wananchi tulioahid kuwatumikia,”amesema.
Naibu Meya huyo alitumia fursa hiyo kuwaomba radhi madiwani alipowakosea ama walipokwazana,kikubwa washirikiane kuhakikisha halmashauri inawahudumia wananchi kwa ufanisi.
Kwa upande wake Katibu wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Deogratius Nakey,amewataka madiwani wame wamoja na waanze upya kuwahudumia wananchi kwa sababu wanawategemea na wanahitaji kupata huduma nzuri, hivyo wakawatimizie mahitaji yao.