Wadau wa sekta ya michezo nchini wamealikwa kufuatilia mashindano ya The Angeline Jimbo Cup yanayoendeshwa na mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt Angeline Mabula ili kubaini na kusajili wachezaji watakaotumika katika vilabu vyao
Rai hiyo imetolewa na Bi Regina Lubala kutoka ofisi ya mbunge wa Jimbo hilo ambapo amefafanua kuwa mashindano hayo yanahusisha wachezaji kutoka kata za maeneo tofauti ya Jimbo hilo hivyo yanaweza kutumika Kama sehemu ya kuona na kusajili wachezaji kwa vilabu vya ligi za madaraja mbalimbali nchini
‘.. Niwaombe wadau kuja kushuhudia mashindano haya kwani kupitia michezo hii wanaweza kupata wachezaji wazuri kwaajili ya timu zao ..’ Alisema
Aidha Bi Regina amezipongeza timu zinazoshiriki mashindano hayo kwa hatua ya mtoano pamoja na kuzitaka kucheza kwa amani na upendo kwa kuwa michezo si uadui na inaweza kuwa sehemu ya kuwainua kiuchumi
Kwa upande wake nahodha wa timu ya kata ya Ilemela Ndugu Elikana Sanya mbali na kumpongeza mbunge wa Jimbo la Ilemela kwa kuendesha mashindano hayo ameongeza kuwa timu yake imeshindwa kupata ushindi dhidi ya timu ya kata ya Nyakato kwakuwa mpira ni mchezo wa makosa hivyo kushindwa kuzingatia maelekezo ya mwalimu kumewafanya kupoteza mchezo huo huku akiahidi kufanya vizuri katika msimu ujao
Wakati nahodha wa timu ya kata ya Nyakato Ndugu Edwin Isack Yambundo amefafanua kuwa mchezo wa leo ulikuwa lazima watoke na ushindi kwa kuwa wapo katika hatua ya mtoano anaefungwa anaondoka hivyo walimsikiliza mwalimu wao na kujituma kwa bidii pamoja na kujihakikishia kuchukua ubingwa wa mashindano hayo kwa msimu huu wa nane
Timu ya kata ya Nyakato na Timu ya kata ya Ilemela Leo jumanne Septemba 10, zimechuana vikali katika uwanja wa sabasaba ambapo mpaka tamati ya dakika 90 timu ya kata ya Nyakato imeweza kuibuka na ushindi wa magoli matatu dhidi ya goli moja lililofungwa na Timu ya kata ya Ilemela