Happy Lazaro,Arusha .
Arusha .WATAALAMU wa nishati ya umeme kutoka nchi 13 za Mashariki mwa Afrika wamekutana jiji Arusha kwa lengo la kujadili mahitaji ya umeme katika kipindi cha miaka 50 ijayo na namna ya kuvitumia vyanzo vipya vya nishati hiyo ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Msimamizi wa mafunzo hayo Kanda ya Afrika ,Dennis Mwalongo amesema wataalam hao kutoka nchi wanachama wa Easterm Africa Power Pool (EAPP) watajadili kwa wiki mbili namna ya upatikanaji wa nishati ya umeme kupitia vyanzo mbalimbali vya asili ikiwemo joto la Ardhi.
“Wataalamu hawa wamekutana kwa ajili ya kujadili mahitaji ya umeme kwa kanda ya Mashariki katika kipindi cha miaka 50 ijayo ukizingatia kwamba matimizi ya umeme katika kanda ya Afrika Mashariki yamekuwa makubwa kwa sababu watu wanaongezeka”
Mwalongo amesema mafunzo hayo ya wataalamu wa nishati ya umeme,yameandaliwa na shirika la Kimataifa la nishati za Atomic pamoja na EAPP na watajadili pia makadirio ya mahitaji ya umeme katika kipindi cha miaka 50 ijayo kwa kutumia data za kidemographics (idadi ya watu) .
Alizitaja baadhi ya nchi wanachama Kama Ethiopia na Kenya ambazo zimepiga hatua kubwa katika vyanzo vikubwa vya nishati ya umeme na kuweza kuuza umeme kwa nchi nyingine jambo ambalo wataalamu hao watajadili na kuibuka na majibu ya jinsi gani nchi zingine wanachama zinaweza kuwa na vyanzo vya nishati.
Kwa upande wake Katibu mkuu wa shirika la EAPP,James Wahogo amesema nchi wanachama wa EAPP zinauzalishaji Mkubwa wa umeme na wataangalia namna ya nchi hizo ziweze kupeana umeme kwa kuuziana.
“Tanzania imepiga hatua kubwa katika suala la uzalishaji wa nishati ya umeme kutoka vyanzo asili ikiwemo Gesi na tunaimani katika kipindi cha mbeleni itakuwa na umeme mwingi wa ziada na kuziuzia nchi za jirani”amesema Wahogo.
Wahogo alizitaja nchi hizo zinazounda umoja wa EAPP kuwa ni Burundi,Comoro, DRC Congo,Djibouti, Misri,Eritrea,Ethiopia, Kenya,Libya, Madagascar, Malawi,Rwanda,Shelisheli,Sudan Kusini ,Sudan,Tanzania, Uganda na Zambia.
Mmoja ya washiriki kutoka Tanesco idara ya Mipango, Mhandisi Mwandamizi Alex Heruka alisema mafunzo hayo ya kitaalamu yanalenga kufanya makadirio ya matumizi ya umeme kupitia vyanzo mbalimbali vya nishati.
“Ushiriki wetu katika mafunzo haya utasaidia kujifunza makadirio kupitia vyanzo mbalimbali vya kufua umeme kama Maji,Gesi ,Makaa ya Mawe ,Jua ,Upepo Nk na hii itasidia kuepuka athari za mabadiliko ya tabia ya nchi”
Amesema kwa sasa Tanzania imekamilisha kuunganisha mifumo ya umeme kwa kujenga laini za umeme Tanzania kwendq Zambia na ipo katika hatua ya upembuzi akinifu katika nchi za Zambia , Uganda , DRC Congo ,Malawi ,Rwanda na Burundi ili pale panapotokea nchi hizo zinaupungufu wa umeme waweze kuziuzia.