Diwani wa kata ya Kitula Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma Alex Ngui,akizungumza na baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mahilo waliofika kuona maendeleo ya ujenzi wa Zahanati yao.
Na Mwandishi Maalum,Mbinga
WANANCHI wa kijiji cha Mahilo kata ya Kitula Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma,wameiomba Serikali iwasaidie kukamilisha ujenzi wa Zahanati waliyoijenga wao wenyewe ili ianze kutoa huduma na kuwaondolea adha wakiwemo mama wajawazito kutembea umbali mrefu kufuata huduma za kujifungua.
Zahanati hiyo inatarajia kuhudumia zaidi ya wakazi 3,000 wa kijiji hicho kati ya wakazi 9,000 wa kata ya Kitula na hadi sasa imegharimu Sh.milioni 45 kati ya hizo Sh.milioni 13 michango ya wananchi wenyewe,Sh.milioni 28 zimetolewa na Halmashauri ya wilaya Mbinga na ofisi ya Mbunge wa jimbo la Mbinga vijijini imechangia Sh.milioni 4.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao walisema,tangu kijiji hicho kilipoanzishwa hakuna huduma za afya, badala yake wanategemea kupata huduma hizo wilaya jirani ya Nyasa kilometa 20 na Hospitali ya Misheni Litembo iliyopo umbali wa kilometa 15.
Saholo Ndunguru alisema,kukosekana kwa huduma za matibabu baadhi ya wananchi wa kijiji hicho hasa wanawake wajawazito wanalazimika kujifungulia njiani pindi wanapokimbizwa kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma na wengine kupoteza maisha.
Ndunguru alisema,wao kama wananchi wameamua kujenga zahanati kwa nguvu zao ili kuondokana na changamoto hiyo na kilichobaki ni Serikali kufungua na kupeleka watumishi watakao toa huduma kwa wananchi.
Moris Ndunguru alisema,wanawake na watoto wanapata shida kubwa kutokana na kukosa huduma za afya katika kijiji hicho,hivyo wanalazimika kufuata huduma umbali mrefu.
Alisema,kwa muda mrefu wanapata shida kutafuta huduma za afya na akina mama wajawazito wanapoteza maisha wakati na baada ya kujifungua kutokana na kutokuwa na huduma za afya.
“kutokana na shida kubwa tunayoipata tuliamua kutafuta eneo na kufanya usafi kwa ajili ya kujenga zahanati,tumejichangisha fedha sisi wenyewe na kujenga zahanati hii ili tupate huduma karibu,tunaiomba sana Serikali yetu ifanye utaratibu wa kuifungua ili tupate huduma karibu” alisema Ndunguru.
Diwani wa kata ya Kitula Alex Ngui,amewapongeza wananchi wa kijiji hicho kwa uamuzi wa kujenga zahanati ambayo itawasaidia kupata huduma za afya uhakika na karibu na maeneo yao.
Hata hivyo,ameungana na wananchi wa kijiji hicho kuiomba Serikali kuharakisha kufungua zahanati hiyo ili wananchi wapate huduma na kuokoa vifo vinavyotokana na kukosa huduma za afya.
Ngui alisema,zahanati hiyo ilianza kujengwa tangu mwaka 2015 na wananchi wenyewe kwa lengo wapate huduma za afya, lakini walishindwa kukamilisha kutokana na kukosa nguvu ya kifedha,hata hivyo Halmashauri ya wilaya Mbinga ilitoa mifuko 100 ya saruji na bati.
“kata ya Kitula ina watu 9,000 wanaotegemea kupata hudumza za afya kwenye zahanati moja yenye watumishi wawili tu ambao hawawezi kutoa huduma za mama na mtoto badala yake wanatoa huduma za malaria na homa nyingine, wananchi hawa ni wengi naiomba sana Serikali iweze kufungua zahanati hii ili kuwaondolea mateso wananchi”alisema Ngui.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya Mbinga George Mhina alisema,Zahanati hiyo itafunguliwa mwezi huu baada ya kukamilisha baadhi ya taratibu za msingi ikiwemo kupata watumishi watakao kwenda kutoa huduma kwa wananchi.
“Sisi kama Halmashauri tunafuatilia maendeleo ya ujenzi wa zahanati ya Mahilo na tumeshatenga fedha kwa ajili ya kununua vifaa tiba na kinachosubiriwa kukamilika kwa taratibu za ujenzi na kupata watoa huduma watakaoletwa na Serikali”alisema Mhina.