Na Zainab Ally – Mikumi.
Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama ya Visiwa vya Shelisheli imevutiwa na Hifadhi ya Taifa Mikumi iliyopo mkoani Morogoro na kuahidi kuwa mabalozi kindakindaki wa kuitangaza hifadhi hiyo inayosifika kwa kuwa na wanyama wanne wakubwa (The big four).
Hayo yamesemwa leo Septemba 6, 2024 na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Fransois Adelaide wakati walipotembelea Hifadhi hiyo na kusema wamevutiwa na kufurahishwa na mandhari nzuri na makundi makubwa ya wanyama waliowaona na kwa ukaribu kitu ambacho watalii wengi hupenda kukishuhudia wanapokuwa hifadhini.
“Kwetu sisi ni mara ya kwanza kuona Simba na Chui, ni jambo la kumshukuru Mungu kwani hatukufikiria kuwa ipo siku moja tutawaona wanyama kama hawa, tunaahidi kuwa tukirudi nyumbani kwetu tutakuwa mabalozi wa kuitangaza Hifadhi hii”, alisema Adelaide.
Alisema mbali na kuwaona Simba na Chui pia wamewaona Tembo na Nyati wanyama ambao ni “Big Four” ambapo aliushukuru uongozi wa Hifadhi ya Taifa Mikumi kwa ukarimu wao na kwamba watakaporejea kwao Shelisheli watahamasisha wananchi wa Taifa lao kuja Tanzania hususan Hifadhi ya Taifa Mikumi kufanya utalii.
Naye Mjumbe wa kamati hiyo, Audrey Vidot alisema amevutiwa na vivutio vya Hifadhi ya Taifa Mikumi kwani wameona wanyama ambao hapo awali walikuwa wakiwasikia na kuwaona kwenye sinema pekee ambapo alisema Watanzania wana kila sababu ya kujivunia rasilimali walizonazo.
Alisema kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakisikia Tanzania ikisifiwa kwa rasilimali walizonazo na kwamba wamebaini ukweli huo baada ya kufika Tanzania na kufanya utalii katika Hifadhi ya Taifa Mikumi ambapo amewataka watanzania kuendelea kutunza rasilimali zao kwa manufaa ya sasa na ya baadae.
Kwa upande wake Afisa Uhifadhi Mkuu David Kadomo alisema kuwa Uongozi wa Hifadhi ya Taifa Mikumi unashukuru kwa ujio wenu kwani mmetupa mengi ya kujifunza na tuwahakikishie kuwa rasilimali hizi tutazitunza, si kwa manufaa ya watanzania tu bali pia kwa manufaa ya mataifa mengine.
“Sisi kama TANAPA mbali na hifadhi hii ya Mikumi tunasimamia pia hifadhi za Taifa 21 zenye vionjo na vivutio mbalimbali, hivyo tunapenda kuwahamasisha tena mtakapopata nafasi ya kurudi tena Tanzania msisite kutembelea Hifadhi za Nyerere,Udzungwa, Saadani, Serengeti, Ruaha na Katavi,”aliongeza Mhifadhi Kadomo.
Hifadhi ya Taifa Mikumi ni miongoni mwa hifadhi kongwe inayosimamiwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na hivi karibu Agosti 31 ilitimiza miaka 60 tangu kuanzishwa kwake, licha ya ukongwe huo bado imeendelea kuvutia watalii wengi wa ndani na nje kutokana uimalishaji wa miundombinu unaotekelezwa na shirika hilo kila mwaka.