NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi,akifungua Kongamano la Wiki ya Kachorora la kuadhimisha miaka 20 toka kuanzishwa kwa Maskani ya CCM ya Kachorora iliyopo Mwembe Shauri Zanzibar.
AFISA Mwandamizi kutoka Afisi Kuu ya UVCCM Zanzibar Ndugu Shara Ame Ahmed, akitoa mada ya dhana ya kuanzishwa kwa Maskani, katika kongamano la wiki ya Kachorora lililofanyika katika ukumbi wa Kituo cha kulelea Wazee Sebleni Zanzibar.
MJUMBE wa Maskani ya Kachorora Ndugu Suleiman Omar ‘Ganzi’ akitoa nasaha juu ya umuhimu wa Wanachama wa CCM kuwarithisha Watoto itikadi na fikra za ukombozi kabla na baada ya Mapinduzi ili wakue wakijua historia halisi ya nchi.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi,akiwa na Wana Maskani ya Kachorora pamoja na Maskani mbali mbali zilizoalikwa katika hafla hiyo, wakifuatilia kwa makini mada mbali mbali zinazowasilishwa katika kongamano hilo la Wiki ya Kachorora, lililofanyika ukumbi wa Sebleni Wilaya ya Amani kichama Zanzibar.
***********************************
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi,amesema siasa za ulaghai na uchochezi wa vurugu zinazofanywa na upinzani visiwani Zanzibar, hazitozuia ushindi wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Amesema Chama cha Mapinduzi kitapata ushindi wa kihistoria kwa majimbo ya Unguja na Pemba ambao haujawahi kutokea toka kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992.
Kauli hiyo ameitoa wakati akifungua kongamano la wiki ya Kachorora lililofanyika katika ukumbi wa Kituo cha kulelea Wazee Sebleni Wilaya ya Amani kichama Zanzibar.
Alisema ushindi huo utapatikana kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwa wananchi wote mijini na vijijini , ambao kila mwananchi kwa sasa ananufaika na huduma muhimu za kijamii zilizoimarishwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alieleza kuwa hakuna chama cha siasa chochote duniani kilichopata kibali na ridhaa ya kuongoza dola kupitia njia ovu za vurugu,vitisho na uongo badala yake vyama vinavyoongoza dola ni vile vilivyokuwa karibu na wananchi kutokana na uhodari wa kutekeleza kwa vitendo matakwa ya wananchi.
Dk.Mabodi, alifafanua kuwa CCM itaendelea kuweka vipaumbele vya kuisimamia serikali itekeleze kwa vitendo sera za maendeleo kwa wananchi,huku wapinzani wakiendelea kujinadi na kupiga porojo zisizokuwa na tija kwa wananchi.
“Chama cha Mapinduzi hakitishwi na hakiogopi taasisi yoyote ya kisiasa wala kundi la watu , kwani ni chama imara na chenye historia kubwa barani Afrika na Duniani kote hivyo hao walioanza kujitokeza kuleta uchochezi tunawaonya waache kuchafua nchi vinginevyo watajuta kwa uovu wao.
Nawambia kwamba ushindi wetu ni lazima kama Ibara ya 5 ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo jipya la 2017 inavyoelekeza, sasa tuwaone na uchaguzi huu watakuja na uongo upi kwani uchaguzi uliopita waliiba kura na kuvuruga uchaguzi na uchaguzi wa marudi wakasusia.”,alisema Dk.Mabodi.
Kupitia kongamano hilo alivitaka vyombo vya Ulinzi na Usalama nchini kutekeleza wajibu wao kwa kudhibiti uvunjifu wa amani na utulivu, ulioanza kuvunjwa na baadhi ya wanasiasa wanaotamka kauli za uchochezi bila kuchukuliwa hatua za kisheria.
Alisema Chama cha Mapinduzi kwa muda mrefu kimekuwa na uvumilifu wa kisiasa kwa kuheshimu sheria,miongozo na kanuni za Uchaguzi na nchi lakini hakitokuwa tayari kuona baadhi ya wanasiasa wanaibuka na kuhamasisha vurugu.
“Itafikia wakati uvumilivu wetu utakuwa na kikomo kama vyombo vya ulinzi na usalama mtashindwa kuwadhibiti hao wanaofanya vurugu wakiweka mguu wa kushoto na sisi tutaweka mguu wa kulia, nchi haitakalika na hatutaki kufikia huko bali tushindane kwa hoja na sera za kimaendeleo.”, alisisitiza Naibu Katibu Mkuu huyo.
Aliwambia wanachama wa CCM walioshiriki katika Kongamano hilo kuwa wanatakiwa kuwahamasisha wananchama wenzao na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi la uandikishaji wa daftari la wapiga kura linalotarajiwa kuanza Januari 18 kisiwani Pemba.
Alisema ushiriki wa Wana CCM katika zoezi hilo la Daftari la wapiga kura ni sehemu muhimu ya kuandaa mazingira ya ushindi wa CCM kwani ndio chimbuko la kupatikana wapiga kura watakaofanikisha ushindi wa CCM uchaguzi mkuu ujao.
Katika maelezo yake Dk.Mabodi,aliwataka Wabunge, Wawakilishi na Madiwani kufanya mikutano ya Hadhara katika maeneo yao na kueleza kwa kina namna walivyotekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020.
Akizungumzia umuhimu wa maskani Dk.Mabodi, alisema maskani ni sehemu ya kueneza itikadi na kupanga Mapinduzi ya kiuchumi yenye kuleta maendeleo endelevu.
Alisema viongozi namba moja ndani ya Chama cha Mapinduzi ni mabalozi wa mashina na maskani hivyo ni lazima viongozi washuke katika ngazi hizo kufahamu mahitaji yao na kupokea ushauri wa kujenga chama.
Aliwapongeza Wana Maskani ya kachorora kwa ubunifu wao wa kuandaa kongamano la kujadili masuala muhumu ya kujenga chama sambamba na kuzialika maskani zingine ili kuendeleza umoja na mshikamano.
“Maskani ya kachorora ni kati ya maskani kubwa tatu Tanzania zilizofanya mambo makubwa nchini na zenye historia ya chimbuko la kueneza itikadi na miongozo imara ndani nan je ya chama chetu”, alisema.
Dk.Mabodi, aliwapongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli kwa uchapakazi wao mzuri
Naye Katibu wa Maskani ya Kachorora ndugu Samia Leonard Shirima,alisema lengo la kufanya kongamano hilo ni kutoa elimu ya juu ya masuala mbali mbali yanayotekezwa na CCM pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aidha,alisema makani hiyo inasherehekea miaka 20 toka kuanzishwa kwake hivyo inafanya shughuli mbali mbali za kijamii zikiwemo kufanya usafi,kutembelea viongozi wastaafu na wazee wa Chama cha Mapjnduzi.
Katika kongamano hilo la siku moja zilizotolewa mada tatu zikiwemo unyanyasaji wa kijisia, dhana ya kuanzishwa kwa maskani pamoja na Mafanikio ya awamu ya saba.