Na MWANDISHI WETU
WADAU wa Utalii katika Hifadhi ya Taifa Serengeti wameiomba Serikali kupatia suluhisho la kudumu la ujenzi wa barabara katika Hifadhi za Taifa hususani barabara ya Serengeti
Akizungumza leo na waandishi wa habari ambao wametembelea eneo hilo, ambapo Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Wolway Trekking Tanzania Limited, John Macha alipongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali kupitia TANAPA katika kuboresha barabara hizo ambazo kwa kiasi kikubwa ziliathiriwa kwa kiasi kikubwa na mvua zilizonyeesha mwanzoni mwaka huu.
Macha aliyasema hayo mbele ya Kamishna ya Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Juma Kuji, ambaye alifanya ziara ya kukagua matengenezo ya muda mfupi ya barabara hiyo.
Kutokana na hali hiyo wadau hao wamependekeza kujengwa kwa barabara yenye tabaka gumu katika hifadhi hiyo ikiwa ni mwarobaini wa tatizo la barabara.
“Niipongeze Serikali kwa matengenezo haya ya barabara kutoka Seronera mpaka Golini tunafahamu hii ni kazi kubwa mnaifanya na tunaomba muendelee nayo lakini kwa ufumbuzi wa kudumu kuwe na jawabu la kudumu kwa sababu magari ni mengi mtakuwa mnafanya zoezi hili ndani ya wiki mbili mpaka tatu mnarudia zoezi hili.
“Kwa hiyo lile wazo Serikali kupitia Serengeti la kuwa na tabaka gumu la kudumu lingekuwa wazo zuri sana wakati huu tungesahau matengenezo haya ya mara kwa mara na hata kuongeza gharama ni bora tuingie gharama kutengeneza barabara itakayokaa muda mrefu hata kama ni gharama kubwa,” alisema Macha
Januari 26, 2024Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Juma Kuji alifanya ziara ya kukagua miundombinu katika Hifadhi ya Taifa Serengeti na kuiagiza menejimenti ya hifadhi hiyo, kushughulikia kwa haraka maeneo korofi ya barabara ndani ya hifadhi ili watalii wafikie azma yao ya kutembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Kutokana na hali hiyo aliilekeza Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Serengeti kurekebisha maeneo yote korofi na kuhakikisha kuwa hakuna maeneo ambayo hayatapitika licha ya uwepo wa mvua kubwa zinazoendelea kunyesha ili kupunguza adha kwa wageni.
“Licha ya changamoto ya mvua kubwa zinazoendelea hatuwezi kusubiri ziishe tumeazimia kushughulikia kwa haraka maeneo yote korofi ikiwa ni hatua za haraka, lakini lengo kuu ni kuhakikisha barabara hizi zinakuwa na tabaka gumu, haya ni maagizo yangu kwa menejimenti kuhakikisha barabara zote zinapitika wakati wote,” alisema Kamishna Kuji.
Aidha, alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya kukarabati miundombinu ambayo kwa kiasi kikubwa imeathiriwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchi nzima.
Pamoja na hali hiyo, Kamishna Kuji amebainisha kuwa TANAPA imejipanga kuhakikisha miundombinu yote katika Hifadhi za Taifa nchini inaboreshwa ili kukidhi matamanio ya wageni wanaotembelea hifadhi hizo zilizosheheni sifa lukuki za kuwa na utajiri mwingi wa bayoanuai.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi anayeshughulikia miundombinu Mhandisi Dkt. Richard Matolo alibainisha kuwa Shirika limekuwa likitumia teknolojia mbalimbali kutafuta mwarobaini wa changamoto za barabara na kubainisha kuwa mwaka huu hali imekuwa tofauti kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha tofauti na miaka mingine.
“Shirika limefanya majaribio mbalimbali na kuja na teknolojia ambazo zitapelekea barabara hizi hususani hii ya Naabi iwe inapitika wakati wote tafiti nyingi zilionekana haziwezi kuleta matokeo chanya katika maeneo haya kutokana na asili ya udongo wa hifadhi zetu hivyo kutokana na stadi zote imethibitika kuwa tunaweza kutumia tabaka gumu kujenga barabara hizi,” alisema
Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Moronda Moronda alisema kuwa menejimenti ya Serengeti imejipanga kuhakikisha maeneo korofi yanarekebishwa na kutoa rai kwa waongoza watalii kuzingatia sheria na taratibu mbalimbali katika hifadhi ikiwemo alama mbalimbali za barababra ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza hasa wakati huu wa mvua.
Hifadhi ya Taifa Serengeti hivi karibuni imekumbwa na changamoto ya barabara kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha Tanzania na nchi jirani, hivyo ukarabati wa miundombinu ya barabara hizo unaofanywa na TANAPA utaondoa adha hiyo na kuzifanya barabara za hifadhi za Hifadhi ya Taifa Serengeti kupitika mwaka mzima.