Waziri wa habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita akikagua maeneo ya mbali mbali ya ujenzi ndani ya Uwanja wa New Amani Complex ikiwa ni hatua ya pili ya ujenzi wa mradi huo.
Na Sabiha Khamis Maelezo
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita amewataka wafanyabiashara kujitokeza kwa wingi kupeleka barua za maombi ya kukodi maduka ya Uwanja wa New Amani Complex.
Ametoa wito huo wakati akikagua ujenzi wa majengo hayo huko Amani Wilaya ya Mjini, amesema miradi hiyo imekamilika kwa kiwango kikubwa.
“Nmeridhishwa na hatua ya pili ya ujenzi na ukarabati wa mradi huu wa maeneo yaliomo katika Uwanja wa Amani ambao umeweza kukamilika kwa asilimia 99” alisema Waziri Tabia.
Amesema kutakuwa na utaratibu maalum wa kuchagua aina za biashara ambazo zitauzwa katika maduka hayo na wafanyabiashara wa vifaa vya michezo watapewa kipaumbele.
Amefafanua kuwa hatua iliyofikia hivi sasa ni pamoja na kurekebisha mapungufu madogo madogo yakiwemo kuziba nyufa pamoja na uwekaji wa vifaa kwa kutumia mashine na uingizaji wa thamani (funiture).
Aidha amesema mradi huo unategemewa kukamilika ndani ya mwezi huu na kukabidhiwa kwa Wizara ili taratibu nyengine za kiserikali ziendelee ikiwemo kufunguzi na uzinduzi wa majengo hayo.
“Tunategemea ndani ya tarehe 19 ya mwezi huu mradi huu utakabidhiwa rasmi kutoka kwa mkandarasi na kuja kwetu Wizara” alisema Waziri Tabia.
Hata hivyo Waziri Tabia ameeleza kuwa amekagua maeneo ya mbele ya maduka ambayo kwa muda mrefu hayakufanyiwa marekebisho ambapo kwa sasa yamekamilika ingwa kuna mapungufu madogo madogo ikiwemo ubora na umadhubuti wa mabati ya mapaa.
Aidha amewataka wakandarasi wa Kampuni ya Orgun kufanya marekebisho ya mabati hayo ndani ya wiki moja kwa kuweka mabati imara ili kuendelea na utaratibu wa kukodisha maduka hayo kwa ajili ya kupata kipato katika Wizara na Serikali kwa ujumla.
Mradi wa ujenzi huo umekusanya maeneo mbali mbali ikiwemo Hoteli, Ukumbi wa mikutano ya kimataifa, Mkahawa na ukumbi wa kuchezea michezo ya ndani (in door games).