NA FAUZIA MUSSA
MKURUGENZI Mkuu Taasisi ya Utafi wa Kilimo Zanzibar (ZARI), Dk. Mohamed Dhamir Kombo, amewataka wakulima wa mbogamboga kuyatumia mafunzo wanayopatiwa ili kuongeza uzalishaji.
Akizungumza na wakulima hao, wakati akifungua Mafunzo ya utayarishaji wa mbegu bora za zao hilo, katika ukumbi wa Taasisi hiyo Kizimbani, alisema hatua hiyo ni moja ya kuungamkono juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi za kuhakikisha wakulima wadogowadogo wanalima kisasa na kujiongezea kipato ili kujiendeleza kiuchumi na kujikwamua kimaisha.
Alifahamisha kuwa Zanzibar kuna wakulima zaidi ya laki mbili wa mbogamboga ambapo baadhi ya wakulima wa wilaya za unguja wamepata fursa ya kupatiwa mafunzo hayo, ili kuwa mabalozi wa kuineza taaluma hiyo kwa wakulima wenzao na kuwataka kuyatumia ipasavyo ili kufikia malengo yaliokusudiwa.
Alisema mbegu bora za kilimo zinasaidia kuongeza uzalishaji, kuwatoa wakulima katika kilimo cha mazowea na kuwafikikisha katika kilimo cha biashara, hivyo mafunzo hayo yatawawezesha wakulima wadogo wadogo kuweza kujitengenezea mbegu zao wenyewe na kuzitumia katika kilimo chao jambo ambalo litawapunguzia gharama wakati wa uzalishaji.
“endapo mkulima atakua na mbegu bora kutasaidia kuzalisha mazao bora, na kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,mbegu hizi zitawasaidia katika kilimo chao na kuwaingizia kipato kwa kuwauzia wakulima wengine.” Alisema Dk. Dhamir
Mbali na hayo alisema kupatikana kwa mbegu bora kutapelekea kuzalishwa kwa mazao bora yanayosaidia kuimarisha afya za jamii.
Mwezeshaji kutoka chuo cha utafiti Arusha Omar Mbwambo alisema mbegu ni kitu muhimu katika uzalishaji wa zao lolote hivyo kupatikana mbegu bora kutasaidia kupatikana mazao bora.
Alisema uzowefu unaonesha kuwa kupatikana mbegu bora bado ni changamoto kutokana na teknolojia duni ya uazalishaji, udhibiti mbovu baada ya kuvuna ,kukosekana mbegu zinazoshindwa kukabiliana na magonjwa, pamoja na wakulima kutokuwa tayari kukubali aina mpya ya mbegu, hivyo mafunzo hayo yatasaidia kuleta mabadiliko chanya ya kilimo kwa wakulima hao.
Aidha aliwashauri wakulima hao kuvuna mbegu zikiwa zimekomaa kwa kiasi na zilizo katika mmea wenye afya sambamba na kutumia zana stahiki za kuvunia mbegu hizo kulingana na aina ya zao ili kuleta matokeo mazuri katika kilimo.
Mbwambo Aliwasisitiza wakulima hao kuzingatia usafi wakati wa utayarishaji wa mbegu na kuondoa vitu visivyohitajika ikiwemo mbegu zilizovunjika,magugu pamoja na mabaki ya mmea ili kuongeza ubora na kiwango cha utoaji wa mbegu.
Mkulima wa kilimo cha matunda na mbogamboga shehia ya Binguni wilaya ya Kati,Namri Najim Jecha, alisema umefika wakati sasa kwa wakulima wadogo wadogo kuzalisha mbegu zao wenyewe ili kupunguza gharama na kuwa na uhakika na usalama wa mbegu hizo.
“mbegu kama F1 zinauzwa kwa bei kubwa , na wakulima wadogowadogo kipato chatu ni cha chini,endapo tutatengeneza mbegu zetu wenyewe kutasaidia kuzipata kwa gharama nafuu na kuwana mbezenye uhakika nazo.” Alisema mkulima huyo
alisema wakulima wengi wamekuwa wakipata hasara kwa kununua mbegu zisizoota kutokana na kukaa muda mrefu tangu zilipozalishwa hivyo mafunzo hayo yatawasaidia kuzalisha mbegu bora zinazoendana na wakati.
Jumla ya wakulima 50 wa kilimo cha mboga mboga wa wilaya za Unguja, wamenufaika na Mafunzo hayo yalioandaliwa na taasisi ya utafiti wa Kilimo Zanzibar (ZARI) kwa kushirikiana na Taasisi ya World vegetable Centre ya Arusha kupitia mradi wa matumizi ya mbegu bora na uhifadhi wa afya ya udongo katika kuongeza uzalishaji wa mbogamboga chini ya ufadhili wa shirika la maendeleo la Marekani USAID.